Arobaini wauawa katika mfululizo wa mashambulizi kusini mwa Syria
Imechapishwa:
Watu wasiopungua 40 wameuawa Jumatano wiki hii katika mfululizo wa mashambulizi ya kujitoa mhanga ya kundi la Islamic State katika mkoa wa Soueida unaodhibitiwa na serikali kusini mwa Syria, kwa mujibu wa OSDH.
Kundi la IS limeendesha mashambulizi hayo ambayo pia yamesababisha watu wengi kujeruhiwa, kabla ya kuzindua mashambulizi katika maeneo ya mkoa huo, shirika la Haki za Binadamu nchini Syria (OSDH) limesema.
"Washambuliaji watatu wa kujitoa mhanga walilipua mikanda yao iliyokua imejaa vilipuzi katika mji wa Soueida", mji mkuu wa jimbo la Soueida, mkurugenzi wa OSDH, Rami Abdel Rahman, ameliambia shirika la habari la AFP.
Washambuliaji wengine wa kujitoa mhanga waliendesha mashambulizi mengine katika vijiji vya kaskazini-mashariki mwa mkoa huo.
Watu angalau 40, ikiwa ni pamoja na raia na askari wa serikali, wameuawa na wengine zaidi ya 30 wamejeruhiwa, chanzo hicho kimesema.
Mashambulizi haya ni ya kwanza yenye ukubwa huu yanayoendeshwa na IS tangu miezi kadhaa iliyopita nchini Syria, ambako kundi hili limepata pigo kubwa kwa kupoteza maeneo yake muhimu.