AFGHANISTAN-TALIBAN-USALAMA

Askari na polisi zaidi ya 40 wauawa katika shambulio Afghanistan

Mkoa wa Baghlan, Afghanistan.
Mkoa wa Baghlan, Afghanistan. Wikimedia Commons

Serikali ya Afghanistan imepoteza askari na polisi zaidi ya arobani waliouawa katika shambulio la wapiganaji wa Taliban usiku wa kuamkia Jumatano wiki hii dhidi ya kambi ya vikosi vya nchi hiyo katika mkoa wa Baghlan kaskazini mwa nchi, kwa mujibu wa chanzo cha kijeshi.

Matangazo ya kibiashara

Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan haijatoa maelezo yoyote kuhusiana na shambulio hilo. Lakini viongozi wa mkoa wa Baghan wanasema polisi tisa na askari 35 waliuawa katika shambulio hilo.

Shambulio dhidi ya kambi hiyo ni pamoja na shinikizo kubwa ambalo kundi la Taliban linaendelea kutoa kwa majeshi ya serikali.

Siku ya Jumatatu wapiganaji wa Taliban walishambulia kambi ya kijeshi katika mkoa wa Faryab, kaskazini mwa nchi.

Katika Ghazni, katikati mwa nchi, hali inaonekana kuimarika leo Jumatano baada ya siku tano za mapigano kati ya wapiganaji wa Taliban na vikosi vya serikali, vikisaidiwa na vikosi maalum vya Marekani ikiwa ni pamoja na ndege za kivita za Marekani.

Uongozi wa kijeshi wa Taliban umeamuru wapiganaji wake kuondoka mji huo, ulio kwenye umbali wa kilomita 150 kusini magharibi mwa Kabul.

Mapigano hayo yamesababisha mamia ya watu kupoteza maisha na wengine kujeruhiw na kusababisha uharibifu mkubwa wa majengo na vifaa mbalimbali.

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imetangaza kuwa itapeleka dawa na vifaa katika hospitali zya mji huo. Vifaa vya maji na jenereta pia zimetolewa.