AFGHANISTAN-USALAMA

Arobaini na nane wauawa kwa Bomu Afghanstan

Watu 48 wameuawa na 67 wamejeruhiwa katika shambulio la kujitoa muhanga lililolenga kituo cha elimu ya ziada katika eneo linalokaliwa na watu wengi kutoka jamii ya Mashia, Wizara ya Afya ya Afghanistan imesema.

Polisi  wa Afghanistan akifika katika eneo la latukio huko Kabul, Agosti 15, 2018.
Polisi wa Afghanistan akifika katika eneo la latukio huko Kabul, Agosti 15, 2018. REUTERS/Omar Sobhani
Matangazo ya kibiashara

Waathirika wote ni raia wa kawaida, wanafunzi wa shule ya sekondari ambao walikua wakipata mafunzo ya ziada, wakijiandaa kufanya mtihani wa kuingia Chuo Kikuu.

Haijajulikana ni kundi gani limetekeleza mauaji haya. Lakini mashambulizi yaliyosababisha vifo vingi katika mji mkuu na mashariki mwa nchi katika miezi ya hivi karibuni yalidaiwa kutekelezwa na kundi la Islamic State.

Serikali ya Marekani imelaani tukio hilo.Tukio hili linarejesha nyuma harakati za kuleta amani ya kudumu ya taifa hilo, imesema ikulu ya White house katika taarifa yake.

Kituo cha shule cha Mawoud kilikuwa kimejaa wanafunzi wengi Jumatano alasiri wiki hii. Wanafunzi zaidi ya mia moja, wasichana na wavulana, walikuwa wakipata mafunzo ya ziada, wakijiandaa kufanya mtihani wa Kankor, unaowaopa fursa ya kuingia katika Chuo Kikuu nchini Afghanistan, wakati mshambuliaji wa kujitoa muhanga alipojilipua.

Hayo yanajiri wakati ambapo polisi 35 waliuawa pia katika shambulio jingine kaskazini mwa Banglan.