Watu 11 wauawa katika shambulizi la kujitoa mhanga Iraq
Imechapishwa:
Watu wasiopungua 11 wameuawa, ikiwa ni pamoja na maafisa wa usalama, katika shambulizi la kujitoa mhanga katika kituo cha Qaïm, mji ulio kwenye umbali wa kilomita 340 magharibi mwa Baghdad, kwa mujibu wa polisi.
Shambulizi hilo lililotokea mapema asubuhi, pia liliwajeruhi maafisa watano wa usalama na raia 11, Mahmoud Jassem, afisa wa polisi ameliambia shirika la Habari la AFP.
Askari wawili na maafisa watatu wa Hashd al-Shabi, kundi lililosadia jeshi kulitimuakundi lenye msimamo mkali wa kidini la Islamic State (IS), ni miongoni mwa watu waliouawa.
Vikosi vya Serikali vilidhibiti mji wa Al-Qaim mnamo mwezi Novemba 2017, moja ya ngome za mwisho inayoshikiliwa na kundi la IS.
Mwezi mmoja baadaye, Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi alitangaza kumalizika kwa vita lakini, kwa mujibu wa wataalamu, wanamgambo wa kundi la Islamic State bado wanajificha pembezoni mwa mpaka na katika jangwa kubwa la Iraq.