UTURUKI-MAREKANI-SAUDI ARABIA-JAMAL-HAKI

Rais wa Uturuki kuweka wazi mkasa ulimtokea Jamal Khashoggi

Wanaharakati wa haki za binadamu na ndugu na marafiki wa mwandishi kutoka Saudi Arabia, Jamal Khashoggi wakiandamana mbele ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia Oktoba 8, 2018.
Wanaharakati wa haki za binadamu na ndugu na marafiki wa mwandishi kutoka Saudi Arabia, Jamal Khashoggi wakiandamana mbele ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia Oktoba 8, 2018. ©REUTERS/Murad Sezer

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, hii leo anatarajiwa kuweka wazi kile alichosema mwishoni mwa juma lililopita kuwa, ni ukweli kuhusu mazingira ya namna mwandishi wa habari Jamal Khashoggi aliuawa ndani ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Instanbul.

Matangazo ya kibiashara

Hotuba ya rais Erdogan inakuja wakati huu rais wa Marekani, Donald Trump akisema hajaridhishwa na maelezo yaliyotolewa na utawala wa Riyadhi kuhusu kifo cha mwanahabari huyo ambapo pia amemtuma mkurugenzi wake wa shirika la Ujasusi FBI kuonana na mwanamfalme Salman.

Kwa sasa dunia inategemea matokeo ya uchunguzi wa vyombo vya usalama vya Uturuki waliofanya juma lililopita kubaini ukweli wa tukio lenyewe.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, mashirika ya kutetea haki za binadamu na vyama vya waandishi wa habari vimetaka waliohusika na mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi nchini Uturuki waadhibiwe.

Hivi karibuni Saudi Arabia ilikiri kuwa Khashoggi alifikwa na umauti kwenye ubalozi wake mdogo alipokuwa akijaribu kupigana na maafisa kwenye ubalozi huyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la Saudi Arabia (SPA) mabishano kati ya Jamal Khashoggi na watu aliokutana nao kwenye ubalozi huo mdogo yaligeuka na kuanza kurushiana makonde ugomvi ambao ulisababisha kifo chake.

Taarifa ya vyombo vya habari vya serikali nchini Saudi Arabia imeongeza kusema kuwa mshauri wa mahakama ya Saudi Arabia, Saud al-Qahtani na naibu Mkuu wa idara ya upelelezi Ahmed Asiri wamefukuzwa kazi.

Vyombo vya habari vya serikali ya Uturuki vimekuwa vikidai mara kwa mara kwamba Khashoggi aliteswa na kuuawa na kuchinjwa na kikosi cha makatili wa Saudi Arabia ndani ya ubalozi, lakini Uturuki inatarajia kueka wazi tukio hilo leo Jumanne.

Saudi Arabia hapo awali ilizikanusha tuhuma kwamba Khashoggi aliuawa katika ubalozi wake mdogo na kuzitaja tuhuma hizo kuwa hazina maana. Vyombo vya habari vya serikali ya Saudi Arabia pia vilipuuza madai kutoka kwa maofisa wa Uturuki kuwa kikosi cha Saudi "cha mauaji," ikiwa ni pamoja na afisa mmoja kati ya washirika wa ndani wa mwana mfalme Mohammed bin Salman na mtaalam wa kuchunguza maiti  kilikwenda mapema na kumsubiri Khashoggi ndani ya ubalozi huo mdogo mjini Istanbul.

Kabla ya Saudi Arabia kutoa taarifa hiyo, rais wa Marekani Donald Trump alisema anaweza kuzingatia kuiwekea vikwazo Saudi Arabia lakini wakati huo huo amesisitiza umuhimu wa uhusiano wa nchi hizo mbili. Trump amesema maelezo yaliyotolewa na Saudi Arabia ni ya kuaminika.

Khashoggi, aliyekuwa mkosoaji mkuu wa sera ya mwana mfalme Mohammed bin Salman, alitoweka baada ya kuingia ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul mnamo tarehe 2 mwezi huu kwa ajili ya kupata hati ambayo ingelimwezesha kufunga ndoa na mchumba wake wa Kituruki.