SAUDI ARABIA-HAKI ZA BINADAMU-MAUAJI

Hali ya haki za binadamu nchini Saudi Arabia kujadiliwa Uswisi

Waandamanaji wakisafiri kwa basi wakielekea kushiriki maandamano dhoidi ya mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi, London, Oktoba 25, 2018.
Waandamanaji wakisafiri kwa basi wakielekea kushiriki maandamano dhoidi ya mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi, London, Oktoba 25, 2018. Reuters/路透社

Wawakilishi wa mataifa mbalimbali wanakutana leo jijini Geneva nchini Uswizi, kujadili hali ya haki za binadamu nchini Saudi Arabia. Mkutano huu unafanyika wakati huu, Jumuiya ya kimataifa ikitaka majibu kutoka kwa uongozi wa Saudi Arabia kuhusu kifo cha Jamal Khashoggi.

Matangazo ya kibiashara

Wiki iliyopita, taarifa rasmi kutoka kwa kiongozi wa mashtaka nchini Uturuki, ilieleza kuwa Khashoogi alinyongwa hadi kufa katika mauaji yaliyopangwa.

Ofisi ya Mkuu wa Mashtaka ya umma ilisema kuwa, baada ya Khashoggi kunyongwa, mwili wake ulikatwakatwa.

Bw Khashoggi, mkosoaji wa Serikali ya Saudi Arabia, alitoweka tarehe mbili Oktoba baada ya kuingia ubalozi wa Saudia mjini Istanbul.

Saudi Arabia inasema kuwa madai kuwa iliamrisha kuuliwa kwa Bw Khashoggi si ya ukweli.

Uturuki inadai kuwa ina sauti na video zinazoonyesha kuwa mwandishi wa habari raia wa Saudi Arabia aliuawa ndani ya ubalozi wa Saudi Arabia nchini Istanbul mapema mwezi huu kwa mujibu wa maafisa wa Marekani na Uturuki walionukuliwa na gazeti la Washington Post.

Mwandishi huyo Jamal Khashoggi aliingia katika ubalozi huo ulio mjini Istanbul tarehe mbili Oktoba kwa minajili ya kupata stakabadhi ambazo zingemruhusu amuoe mchumba wake raia wa uturuki. Hajaonekana tangu wakati huo.

Sauti zilizorekodiwa zinatoa ushahidi kuwa kikosi cha watu kutoka nchini Saudi Arabia, kilichotumwa kwenda Istanbul kilihusika katika kumuua Khashoggi.