MAREKANI-SAUDI ARABIA-JAMAL-HAKI

Mauaji ya Khashoggi: Uhusiano kati ya Marekani na Saudi Arabia waendelea kuimarika

Rais wa Marekani Donald Trump katika ikulu ya White House Novemba 20, 2018.
Rais wa Marekani Donald Trump katika ikulu ya White House Novemba 20, 2018. REUTERS/Leah Millis

Rais wa Marekeni Donald Trump ametetea ushirikiano wa nchi yake na Saudi Arabia, licha ya shutuma za kimataifa kwa nchi hiyo kuhusika na mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi.

Matangazo ya kibiashara

Trump katika taarifa yake ya kina kuhusu mauaji ya Khashoggi amesema licha ya mauaji ya Khashoggi hawezi kuharibu uhusiano kati ya Marekani na Saudi Arabia.

Katika ripoti yake, Trump amesema, huenda Mwanafalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman alifahamu au hakufahamu mauaji ya Khassoggi na hivyo, serikali haiwezi kuichukulia hatua yoyote Saudi Arabia.

Trump amesema, amechukua uamuzi huo kwa sababu ya maslahi ya Marekani, kwani Saudi Arabia ni mshirika wa karibu na wa siku nyingi, ambaye anamnufaisha kibiashara.

Uamuzi huu wa rais Trump umewakasirisha wanasiasa wa Marekani ambao wamesema wataendelea kushinikiza ili ukweli ubainike kuhusu mauaji ya Khashogii.

Ripoti ya Shirika la Ujasusi nchini humo CIA, hivi karibuni lilitoa ripoti inayoeleza kuwa viongozi wa Saudi Arabia walifahamu kuhusu kuuawa kwa Khasaggi, aliyekuwa anaandika makala katika Gazeti la Washington post kuukosoa uongozi wa Saudi Arabia.