AFGHANISTAN-IS-TALIBAN-USALAMA

Zaidi ya hamsini wauawa katika shambulio Kabul

Mmoja kati ya majeruhi akipelekwa hospitali baada ya shambulizi la kujitoa mhanga lililoua watu zaidi ya 50 mjini Kabul, Novemba 20, 2018.
Mmoja kati ya majeruhi akipelekwa hospitali baada ya shambulizi la kujitoa mhanga lililoua watu zaidi ya 50 mjini Kabul, Novemba 20, 2018. REUTERS/Mohammad Ismail

Watu zaidi ya 50 wameuawa na 80 wamejeruhiwa katika shambulio la kujitoa mhanga wakati wa mkutano wa kidini wa viongozi wa juu ambao wamekuwa wakisherehekea siku ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad Jumanne wiki hii mjini Kabul, nchini Afghanistan, maafisa wa serikali wamesema.

Matangazo ya kibiashara

Sherehe ya kidini ilikuwa ndo inaanza wakati mlipuko ulipotokea. Jiongozi mmoja wa kidini alikuwa akisoma Aya za Qorani wakati mshambuliaji wa kujitoa mhanga alipolipua mkanda wake uliojaa vilipuzi, moja kati ya manusura amekiambia kituo kimoja cha televisheni nchini humo, mwandishi wetu huko Kabul, Sonia Ghezali, amearifu. Mamia ya watu walikuwa wamekusanyika katika jengo la Uranus, jengo kubwa na maarufu nchini Afghanistan.

Hata hivyo kwa mujibu wa vyanzo vya usalama idadi ya waliopoteza maisha iliongezeka haraka, kwa sasa zaidi ya 50 waliuawa na karibu 80 walijeruhiwa. "Mshambuliaji wa kujitoa mhanga alijilipua katika jengo la Uranus wedding palace, ambapo viongozi wa kidini walikuwa wamekusanyika leo ili kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad," amesema msemaji wa polisi wa Kabul Basir Mujahid.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi Najib Danish, amethibitisha habari hiyo, akibainisha kuwa "viongozi wa kidini walikuja wakitokea nchi nzima na watu wengine walikuwa wakishiriki katika sherehe hiyo " katika ukumbi wa mikutano.

Kwa mujibu wa mashahidi takriban watu 1000 walikuwepo jengo hilo wakati wa mlipuko.

Hakuna kundi hata moja ambalo limedai kuhusika na shambulizi hilo, lakini kundi la Islamic State (IS) mara kwa mara limekuwa likihusika na mashambulizi ya kujitoa mhanga nchini Afghanistan.

Shambulio hilo linatokea katika mji mkuu wa Afghanistan wakati Zalmay Khalilzad, mjumbe wa Marekani wa amani nchini Afghanistan, anaendelea na kushauriana kwa lengo la mchakato wa amani kati ya serikali na Taliban.