ISRAEL-IRAN-SYRIA-USALAMA

Benjamin Netanyahu: Israeli itaongeza shughuli zake dhidi ya Iran Syria

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. REUTERS/Corinna Kern

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameonya kuwa nchi yake itaongeza shughuli zake dhidi ya vikosi vya Irani nchini Syria baada ya kuondoka askari wa Marekani nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi wa Rais Donald Trump wa kuondoa majeshi ya Marekani nchini Syria, aliotangaza Jumatano wiki hii, unaweza kupelekea Iran kujihusisha zaidi katika masuala ya nchi hiyo kwa kutuma silaha zaidi na wapiganaji, maafisa wa Israeli wamesema.

Taifa la Kiyahudi pia lina hofu kwamba kuondoka kwa jeshi la Marekani nchini Syria kutapunguza shinikizo la kidiplomasia la Washington kwa Urusi, mshirika mkuu wa serikali ya Damascus.

"Tutaendelea kupambana kwa hali na mali dhidi ya jitihada za Iran za kusalia nchini Syria," Benjamin Netanyahu amehakikisha kwenye televisheni ya taifa, akizungumzia mashambulizi ya ndege za Israeli dhidi ya majeshi ya Iran na Hezbollah kutoka Lebanon nchini Syria.

"Hatuna nia ya kupunguza juhudi zetu, tutazidisha na najua kuwa itakuwa ni pamoja na msaada kamili wa Marekani, " Waziri Mkuu wa Israel amesema.

Waziri wa Elimu wa Israel Naftali Bennett amesema kama Donald Trump kwamba Daesh (IS) ilishindwa nchini Syria, "kutokana na msaada mkubwa wa jeshi la Marekani". "Lakini Iran inaendeleza operesheni zake na ni tishio kwa ulimwengu," Benjamin Netanyahu ameongeza.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha Moshe Kahlon, amesema ikiwa uamuzi wa Donald Trump sio "mzuri" kwa Waisraeli, "tunajua pia kuwa usalama wa Israeli uko katika maslahi ya Marekani."