MAREKANI-SYRIA-USALAMA

Marekani yatoa masharti kwa askari wake kuondoka Syria

Rais wa Marekani Donald Trump na Mshauri wa masuala ya usalama wa taifa wa Marekani John Bolton, wakikutana na maafisa kijeshi kabla ya kuzuru kambi ya kijeshi ya Al Asad, Iraq Desemba 26, 2018.
Rais wa Marekani Donald Trump na Mshauri wa masuala ya usalama wa taifa wa Marekani John Bolton, wakikutana na maafisa kijeshi kabla ya kuzuru kambi ya kijeshi ya Al Asad, Iraq Desemba 26, 2018. ©REUTERS/Jonathan Ernst

Mshauri wa masuala ya usalama wa taifa wa Marekani, John Bolton, amesema vikosi vya nchi yake vitaondolewa nchini Syria ikiwa baadhi ya matakwa yake yatafikiwa, kauli inayoashiria kuwa huenda vikachelewa kuondoka.

Matangazo ya kibiashara

Akiwa katika ziara ya kikazi nchini Israel na ambayo itampeleka hadi Uturuki, Bolton amesema ataomba hakikisho kutoka kwa utawala wa Ankara kuwa haitowashambulia wapiganaji wa Kikurdi walioko kaskazini mwa Syria.

Bolton pia amesisitiza kuwa nchi yake inataka kuona vita dhidi ya makundi ya kijihadi kama Islamic State inamalizika na kwamba usalama unarejea katika maeneo mengi ya Syria.

Matamshi ya Bolton yanakuja ikiwa ni majuma kadhaa tu yamepita tangu Rais Donald Trump atangaze mpango wa kuanza kuwaondoa wanajeshi wake nchini Syria, hatua iliyosababisha kujiuzulu kwa maofisa wajuu wa wizara ya ulinzi.