SAUDI ARABIA

Viongozi wa nchi za Kiarabu wakutana kuijadili Iran

Viongozi wa nchi za ghuba wakiwa kwenye mazungumzo kwenye moja ya mikutano yao ya hivi karibuni.
Viongozi wa nchi za ghuba wakiwa kwenye mazungumzo kwenye moja ya mikutano yao ya hivi karibuni. ©REUTERS/Assad Hani

Viongozi wa nchi za kiarabu na wale wa kiislamu wameanza kukutana kwenye mji mtakatifu wa Mecca kwaajili ya mikutano mitatu, wakati huu nchi ya Saudi Arabia ikitafuta uungwaji mkono dhidi ya nchi ya Iran.

Matangazo ya kibiashara

Wakati wa mazungumzo nchi ya Saudi Arabia imeikashifu vikali nchi ya Iran kwa kuingilia masuala ya nchi za ukanda, utawala wa Riyadh ukitaka nchi wanachama kusimama pamoja dhidi ya uchokozi wa Iran.

Wito wa Saudi Arabia umekuja wakati huu mshauri wa masuala ya usalama wa taifa wa Marekani, John Bolton akisema nchi ya Iran ilikuwa nyuma ya jaribio la kuharibu meli nne ikiwemo meli ya mafuta ya Saudi Arabia kwenye pwani ya falme za kiarabu.

Waasi wa Yemen ambao wanasaidiwa na Iran wamezidisha mashambulizi ya kutumia ndege zisizo na rubani, ambapo hivi karibuni walisababisha Saudi Arabia ifunge bomba lake kuu la mafuta.

Saudi Arabia, mshirika mkubwa wa Marekani imeamua kuwakutanisha viongozi wa nchi za kiarabu na wale wa kiislamu kwa mkutano wa dharura kuijadili Iran.

Rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi, Mfalme wa Kuwait, Sheikh Sabah Al-Ahmed Al-Sabah na mkuu mpya wa baraza la kijeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ni miongoni mwa viongozi wanaohudhuria mkutano huu.

Utawala wa Riyadh umeitisha mkutano huu kujadili mzozo wake na nchi ya Iran pamoja na kutafuta mbinu za kuutenga utawala wa Tehran kwa hofu ya kutokea vita.