SAUDI ARABIA-KHASHOGGI-UTURUKI-MAUAJI

Ripoti: Ushahidi wamhusisha MwanaMfalme wa Saudi Arabia na mauaji ya Jamal Khashoggi

Uchunguzi wa watalaam wa Umoja wa Mataifa, unaonesha kuwa kuna ushahidi kuwa MwanaMfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman na maafisa wengine wa serikali walihusika na mauaji ya Mwanahabari Jamal Khashoggi.

Picha ya Mwanahabari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi
Picha ya Mwanahabari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi 路透社
Matangazo ya kibiashara

Mtalaam wa Umoja wa Mataifa aliyeongoza uchunguzi huo Agnes Callamard, katika ripoti yake, ameelezea kuwa ushahidi walioupata unathibitisha kuwa Khashoggi aliuawa katika Ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul nchini Uturukio na waliohusika ni maafisa wa usalama wa Saudi Arabia.

“Haiwezekani kuwa MwanaMfalme Mohammed bin Salman hakufahamu kuhusu kilichotokea, mauaji hayo yanakwenda kinyume na sheria za Kimataifa kwa hivyo, ni vema uchunguzi zaidi kufanyika,” alisema Bi. Callamard

“Hakika kwa uchunguzi wetu, mauaji ya Khashoggi, yalipangwa na yalikuwa yanafahamika vema,” aliongeza.

Aidha, ripoti hiyo, inamtaka Bin Salman kuchunguzwa kutokana na mauji hayo ya Khashoggi kwa sababu ushahidi unaonesha kuwa alifahamu kila kitu.

Imebainika pia kuwa wauaji wa Khasshogi walikuwa washirika wa karibu wa MwanaMfalme Salman, na walinaswa kupitia mkanda wa sauti, wakijadiliana kuhusu mauaji hayo.

Khashoggi raia wa SaudI Arabia aliuawa akiwa na umri wa miaka 58, wakati alipokwenda katika Ubalozi wa nchi yake mwezi Oktoba mwaka 2018, kwenda kutafuta vibali ili kufunga ndoa na mpenzi wake Hatice Cengiz.

Wakati wa uhai wake, alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Saudi Arabia kupitia makala alizokuwa anaandika kupitia Gazeti la Washington Post.

Saudi Arabia imeendelea kukanusha madai ya kuhusika na mauaji ya Khashoggi na tayari imewafungulia kesi washukiwa 11 kwa madai ya kutekeleza mauaji hayo.

Hata hivyo, ripoti ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa kesi dhidi ya washukiwa hao ambao hawajafahamika, haijafikia viwango vya kimataifa vya kisheria vinavyotakiwa.

Mwili wa Khashooggi haujawahi kupatikana.