YEMEN-HAKI

Yemen: Watu 30 wahukumiwa kifo kwa usaliti

Wapiganaji wanaounga mkono waasi wa Houthi karibu na mji mkuu wa Yemeni Sanaa (picha ya kumbukumbu).
Wapiganaji wanaounga mkono waasi wa Houthi karibu na mji mkuu wa Yemeni Sanaa (picha ya kumbukumbu). Mohammed HUWAIS / AFP

Wanafunzi, wanaharakati na wahubiri takribani thelathini wamehukumiwa kifo na mahakma ya jinai ya Sanna, nchini Yemen, kwa "kusaliti nchi yao kwa faida ya nchi za kigeni zinazoendesha mashambulizi", ikimaanisha muungano unaoongozwa na Saudi Arabia.

Matangazo ya kibiashara

Watu thelathini, waliofungwa kwa angalau mwaka mmoja hadi miaka mitatu kwa baadhi, walihukumiwa kifo Jumanne, Julai 9, na Mahakama ya Jinai ya Sanaa. Watuhumiwa hao walikutwa na hatia ya kutoa taarifa kwa nchi za muungano unaoongozwa na Saudi Arabia kuhusu maeneo mbalimbali kwa lengo la kutekeleza mashambulizi ya anga. Watu wengine sita waliachiliwa huru.

Mashirika ya haki za binadamu yamelaani hukumu hiyo na kusem akuwa inakwenda kinyume kanuni za sheria ya jinai nchini humo.

Kwa mujibu wa Radhya Al Mutawakel wa Mouwatana wa shirika la haki za binadamu nchini Yemen, hukumu hii inaonekana ni ulipizaji kisasi. Amelaani hukumu isiyo kuwa ya haki na isio kuwa na msingi wa kisheria: "Wakati mfumo wetu wa mahakama haupo, mahakama hii ya jinai ya Sanaa inaanza kazi leo na kutoa hukumu zisizofaa".

"Ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu"

Katika ukurasa wake wa twitter kwa Kiarabu, shirika la kimataifa la Haki za Binadamu la Amnesty International pia limelaani "hukumu hiyo isiyo ya haki", inayoelezwa kama "ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu" na kuomba kusitishwa kwa hukumu hiyo mara moja kwa mtuhumiwa.