ISRAELI-UCHAGUZI-SIASA

Uchaguzi Mkuu Israeli: Netanyahu na Gantz wakaribiana kwa kura

Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na Jenerali mstaafu Benny Gantz.
Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na Jenerali mstaafu Benny Gantz. JACK GUEZ, Oded Balilty / AFP

Taarifa zinaonyesha kuwa idadi za kura kati ya wagombea wawili Waziri Mkuu anaye maliza muda wake Benjamin Netanyahu na mpinzani wake Benny Gantz zilikuwa zinakaribiana sana Jumanne usiku.

Matangazo ya kibiashara

Matokeo ya uchaguzi huu wa wabunge yanaonyesha kuwa idadi za kura kati ya wagombea wawili Benjamin Netanyahu na Benny Gantz zinakaribiana na ripoti ya kwanza iliyotolewa baada ya zoezi la kupiga kura na kurushwa kwenye vyombo vya habari nchini Israeli inathibitisha.

Chama cha Likud cha Benjamin Netanyahu (cha mrengo wa kulia)) kinaweza kupata kati ya viti 31 hadi 33 kwa jumla ya viti 120 vinavyohitajika bungeni na chama cha mrengo wa kati, Kahol Lavan, cha Bw. Gantz kinaweza kupata kati ya viti 32 na 34.

Hakuna chama kinatarajiwa kupata wingi wa viti bungeni, kwa mujibu wa vyanzo kadhaa kutoka Israeli.

Mnamo mwezi Aprili, chama cha Likud (cha mrengo wa kulia) cha Bw Netanyahu na chama cha mrengo wa kati, Kahol Lavan, cha Bw. Gantz vilipata kila upande viti 35 kwa jumla ya viti 120 katika Bungela Knesset.

Wananchi wa Israeli walipiga kura kwa mara ya pili ndani ya kipindi cha miezi mitano Jumanne wiki hii, baada ya duru ya kwanza ya uchaguzi kufanyika mwezi Aprili ambapo Benjamin Netanyahu alishindwa kuunda serikali ya umoja. Ikiwa matokeo ya kura yatathibitishwa, Bw Netanyahu atakuwa na kibarua kigumu cha kuunda serikali ya umoja. Lakini wakati huu, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu yuko chini ya shinikizo kubwa mno.

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anakabiliwa na kibarua kigumu katika Uchaguzi huu ambao iwapo chama chake kitashinda, ataendelea kuwa Waziri Mkuu aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi katika historia ya nchi hiyo licha ya shutuma za ufisadi zinazomkabili.