MAREKANI-UTURUKI-SYRIA-USALAMA

Mashambulizi ya Uturuki Syria: Donald Trump afuta vikwazo dhidi ya Uturuki

Rais wa Marekani, Donald Trump na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika mkutano wa NATO. (picha ya kumbukumbu)
Rais wa Marekani, Donald Trump na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika mkutano wa NATO. (picha ya kumbukumbu) Tatyana ZENKOVICH / POOL / AF

Rais wa Marekani amesema nchi yake inaondoa vikwazo dhidi ya Uturuki, vilivyotangazwa baada ya nchi hiyo kutuma vikosi vyake Kaskazini mwa Syria kupambana na wapiganaji wa Kikurdi.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii imekuja, baada ya Urusi kukubaliana na Urusi, kutuma wanajeshi zaidi katika mpaka wa Syria na kuongeza muda wa kutoshuhudiwa makabiliano hayo.

Trump amesema sasa ni nafasi ya mtu mwingine kupambana na makundi ya kigaidi nchini Syria, baada ya kuondoa wanajeshi wake Kaskazini mwa Syria.

Wanajeshi wa Urusi wameanza kushika doria Kaskazini mwa Syria chini ya makubaliano mapya na Uturuki ambayo yalianza kutekelezwa jana Jumatano ili kuwarejesha nyuma wapiganaji wa vikosi vya kikurdi kutoka kwenye eneo la mpaka.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema vikosi vyake vilivuka mto Euphrates na kusonga mbele kuelekea mpaka kati ya Uturuki na Syria huku duru kutoka wapiganaji wa Kikurdi zikithibitisha kuwasili kwa wanajeshi wa Urusi katika mji wa Kobane.

Mapema wiki hii Rais Reccep Tayyip Erdogan wa Uturuki na Vladimir Putin wa Urusi walifikia makubaliano ya kushirikiana katika kuyadhibiti maeneo yote ya Kaskazini Mashariki ya mpaka wa Syria.