MAREKANI-IS-SYRIA-IRAQ-USALAMA

Kiongozi wa IS Abu Bakr al-Baghdadi auawa katika shambulio la Marekani

Kiongozi wa IS Abu Bakr al-Baghdadi aliuawa katika shambulio la jeshi la Marekani.
Kiongozi wa IS Abu Bakr al-Baghdadi aliuawa katika shambulio la jeshi la Marekani. © AFP

Rais wa Mareakni Donald Trump ametangaza kifo cha kiongozi mkuu wa kundi la Islamic State (IS), Abu Bakr al-Baghdadi wakati wa operesheni za jeshi la Marekani Kaskazini Magharibi mwa Syria.

Matangazo ya kibiashara

Donald Trump amesema mauaji ya kiongozi huyo aliyetafutwa kwa udi na uvumba ni ushindi mkubwa kimataifa. Taarifa hii imepokelewa kwa shangwe na washirika wa Marekani kutoka Ulaya.

Abu Bakr al-Baghdadi amefariki dunia," Trump amesema katika hotuba aliyoitoa katika Ikulu ya White House.

Rais wa Marekani alieleza kwa kifupi jinsi shambulio hilo lilivyoedeshwa na kikosi cha askari wa Marekani hadi kumkaribia kiongozi huyo wa IS na hivyo kuamua kujilipua, akitumia mkanda wake wa kulipuka.

Abu Bakr al-Baghdadi, mtu aliyesakwa sana na nchi mbalimbali za dunia, alichukuliwa kama mhusika mkuu wa mauaji na mateso ya aina mbalimbali nchini Iraq na Syria na mashambulizi mabaya katika nchi kadhaa.

"Kiongozi" aliyejitangaza mnamo mwaka 2014 na kuongoza kwa mkono wa chuma watu milioni 7 nchini Iraq na Syria, amefariki dunia "kama mbwa," amesema rais wa Marekani.

"Hakufa kama shujaa, alikufa kama mbwa," amesema Donald Trump, na kuongeza kwamba alijilipua mwenyewe kwa mkanda uliojaa vilipuzi wakati alikimbilia katika shimo lililochimbwa kwa usalama wake. Watoto wake watatu walikufa pamoja naye, Trump meongeza.

Saa chache baadaye, vikosi vya Kikurdi vimetangaza kifo cha msemaji wa IS Abu Hassan Al-Muhajir katika shambulilizi jipya lililotokea katika mkoa wa kaskazini wa Aleppo. Shirika la Haki za Binadamu nchini Syria (OSDH) limethibitisha operesheni ya "vikosi vya Marekani kwa ushirikiano na wapiganaji wa Kikurdi.