IRAQ-USALAMA

Watu zaidi ya 30 waangamia kwa siku moja Iraq

Makabiliano kati ya waandamanaji an vikosi vya usalama, Baghdad, Novemba 28, 2019.
Makabiliano kati ya waandamanaji an vikosi vya usalama, Baghdad, Novemba 28, 2019. REUTERS/Khalid al-Mousily

Waandamanaji zaidi ya 30 wameuawa kwa siku moja, Alhamisi, Novemba 28 kusini mwa Iraq, katika makabiliano na vikosi vya usalama. Vurugu hizo zimefikia kiwango cha juu katika siku za hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na machafuko yanayoendelea Baghdad.

Matangazo ya kibiashara

Milio ya risai ilisikika katika mtaa wa Al Rasheed katikati mwa jiji la Baghdad. Kwa siku kadhaa, mtaa huu wa kihistoria katika mji mkuu wa Iraq umechukua sura nyingine ya kivita. "Vikosi vya usalama vinatufyatulia risasi, ikiwa ni pamoja na risasi za moto! Na wanatumia gesi ya machozi, jambo ambalo ni marufuku! ", amesema Ali, 28, ambaye ni miongoni mwa waandamanaji waliojificha nyuso zao kwa kitambaa cheusi.

Wakati huo waandamanaji walishambulia ubalozi mdogo wa Iran na kuuteketeza kwa moto.

Waliolichoma moto jengo la ubalozi mdogo wa Iran katika mji wa Najaf walikuwa wakipiga kelele, wakisema ''ushindi kwa Iraq'', na kuitaka Iran iondoke.

Iran imelaan kuharibiwa kwa ubalozi wake, na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya waliohusika.

Mji mkuu wa Iraq, Baghdad pamoja na maeneo ya kusini mwa mji huo, yameshuhudia ghasia za mitaani mbaya zaidi tangu kupinduliwa kwa rais wa zamani Saddam Hussein mwaka 2003, katika uvamizi ulioongozwa na Marekani.

Kulingana na tathmini ya AFP, watu 380 wameuawa katika machafuko hayo ambayo yameikumba Iraq kwa miezi miwili, na wengine 15,000 wamejeruhiwa.