UNICEF-WATOTO-HAKI

Ripoti: Watoto wanaishi katika mazingira magumu katika maeneo ya mizozo

Maafisa wa idara ya uokoaji wakiokoa watoto baada ya shambulio la anga lililotekelezwa na vikosi vinavyotii serikali ya Syria katika kitongoji cha al-Shaar cha Aleppo, Juni 2, 2014.
Maafisa wa idara ya uokoaji wakiokoa watoto baada ya shambulio la anga lililotekelezwa na vikosi vinavyotii serikali ya Syria katika kitongoji cha al-Shaar cha Aleppo, Juni 2, 2014. REUTERS/Sultan Kitaz

Ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya watoto la UNICEF imebaini kwamba mashambulizi dhidi ya watoto kwenye maeneo yenye mizozo yameongezeka mara tatu katika kipindi cha muongo mmoja uliopita,

Matangazo ya kibiashara

UNICEF imenyooshea kidole mataifa ya Syria, Yemen na Afghanistan kuwa ni nchi ambazo watoto wengi wanakabiliwa na mashambulizi mbalimbali.

Ripoti iliyotolewa leo na UNICEF imeeleza kuwepo zaidi ya visa 170,000 dhidi ya watoto, ambavyo ni sawa na visa 45 kwa siku katika maeneo yenye vita tangu mwaka 2010 katika kipindi cha miaka 10. Miongoni mwa madhila wanayopitia watoto ni pamoja na mauaji, kukatwa viungo, kubakwa, kutekwa, kunyimwa huduma za kibinaadamu, kufanyishwa kazi na mashambulizi dhidi ya shule na hospitali.

Kulingana na takwimu zilizotolewa na UNICEF, zaidi ya watoto milioni 2.5 wanaishi kama wakimbizi nje ya Syria.

"Migogoro na vita duniani vimeongeza na vinaendelea kushuhudiwa na kusababisha hali mbaya ya kibinadamu hususan umwagikaji wa damu. Watoto ndio wenye kuathirika zaidi," Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la UNICEF Henrietta Fore, amesema.

Mwaka 2018 pekee, UNICEF iliorodhesha zaidi ya visa 24,000 vya uhalifu dhidi ya watoto, idadi ambayo ni mara tatu zaidi ya hali ilivyokuwa mwaka 2010.