IRAQ-IRAN-MAREKANI-USALAMA

Iran: Maelfu ya watu wenye hasira waandamana Tehran dhidi ya 'uhalifu' wa Marekani

Raia wa Iran wakiandamana Tehran kupinga mauaji ya kamanda wa juu, Jenerali Qassem Soleimani, aliyeuawa katika shambulio la anga la Marekani, Januari 3, 2020.
Raia wa Iran wakiandamana Tehran kupinga mauaji ya kamanda wa juu, Jenerali Qassem Soleimani, aliyeuawa katika shambulio la anga la Marekani, Januari 3, 2020. © AFP

Maelfu ya watu wenye hasira wamemiminika mitaani jijini Tehran, mji mkuu wa Iran, kulaani kile walichokiita "uhalifu" wa Marekani, baada ya kifo cha kamanda mwandamizi wa jeshi la Iran Jenerali Qassem Soleimani.

Matangazo ya kibiashara

Qassem Soleimani ameuawa katika shambulio la anga la Marekani jijini Baghdad.

Baada ya sala ya Ijumaa, umati wa watu wamejazana kwenye mitaa ya katikati mwa mji mkuu wa Irani, Tehran, wakishikilia mikononi picha za Qassem Soleimani, huku wakitoa maneneo makali dhidi ya Marekani.

Wakati huo huo wafanyakazi wa Marekani katika sekta ya mafuta wamelazimika kuondoka nchini Iraq, wakihofia maisha yao, kwa mujibu wa chanzo kutoka wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq.

Jenerali Soleimani alikuwa mtu mashuhuri kwa utawala wa Iran. Kikosi chake cha Qudsi kilikuwa kinaripoti moja kwa moja kwa kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei na alisifiwa kama shujaa wa kitaifa.

Wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon imesema Rais Donald Trump aliamuru kuuawa kwa Soleimani baada ya kundi la waandamanaji wanaoiunga mkono Iran kuuzingira ubalozi wa Marekani.

Iran.

Kuuawa kwa Jenerali Qassem Soleimani, mkuu wa Jeshi maalum la Iran, kunaashiria kuongezeka kwa mgogoro kati ya Marekani na Iran, ambao umekuwa ukitokota tangu Rais Donald Trump alipojiondoa katika mkataba wa nyuklia wa Iran na kutangaza vikwazo vipya vinavyohujumu uchumi wa nchi hiyo.

Hayo yanajiri wakati Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameapa kulipiza kisasi kifo cha Soleimani, katika ongezeko kubwa zaidi la vita vya uwakala kati ya Iran na Marekani katika ardhi ya Iraq.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Javad Zarif, ametaja hatua hiyo kuwa "hatari na uchokozi wa kishenzi".