IRAN-MAREKANI-IRAQ-USALAMA

Iran yashambulia kambi za jeshi zinazotumiwa na askari wa Marekani

Vikosi vya usalama vya Iraq kwenye kambi ya jeshi ya wa Ain al-Assadiliyolengwa na mashambulizi ya Iran(picha ya kumbukumbu).
Vikosi vya usalama vya Iraq kwenye kambi ya jeshi ya wa Ain al-Assadiliyolengwa na mashambulizi ya Iran(picha ya kumbukumbu). REUTERS/Thaier Al-Sudani

Iran imelipiza kisasi kifo cha Jenerali Qassem Soleimani kwa kushambulia kwa makombora kadhaa kambi mbili za jeshi zinazotumiwa na askari wa Marekani.

Matangazo ya kibiashara

Kambi hizo zilizoshambuliwa ni Ain al-Assad na Erbil, ambazo zinaumiwa na askari wa Marekani nchini Iraq.

Shambulio hilo lilitokea karibu saa 1:30 usiku wa kuamkia leo Jumatano

Katika taarifa, jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limetishia Marekani kuwa iwapo itaishambulia Iran basi itajibu kwa kuishambulia vibaya Marekani.

Jeshi la itikadi la Irani pia limetishia kutekeleza mashambulizi dhidi ya Israeli na "serikali zinazounga mkono Marekani".

"Tunawashauri raia wa Marekani kuwarejesha nyumbani askari wa Marekani (waliotumwa) katika ukanda huu ili kuepusha hasara zaidi na kutokubali maisha ya askari wao kuwa hatarini zaidi kwa chuki inayoendelea kuongezeka ya serikali" Marekani, jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limeongeza.

Runinga ya kitaifa ya Iran imetangaza kuwa shambulio hilo ni la kulipiza kisasi mauaji ya kamanda mkuu Qasem Soleimani aliyeuawa katika shambulio la ndege isiyokuwa na rubani mjini Baghdad, kufuatia agizo la rais wa Marekani Donald Trump.

"Iran imechukua hatua za kujilinda sawa na Kifungu cha 51 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa kwa kushambulia kambi ambayo iliendesha shambulio baya dhidi ya raia na maafisa wetu wa ngazi ya juu," ameandika kwenye akaunti yake ya Twitter Waziri wa Mambo ya Nje wa Irani Mohammad Javad Zarif. Hatutaki vita, lakini tutajihami dhidi ya uchokozi wowote. "

Pentagon inasema kuwa karibu kambi mbili zilishambuliwa, mjini Irbil na Al Asad.

Mashambulio hayo yalifanyika saa kadha baada ya mazishi ya Soleimani.

Shambulio la pili lilifanyika katika mji wa Irbil muda mfupi baada ya roketi ya kwanza kugonga Al-Asad, kituo cha televisheni cha Al Mayadeen kiliripoti.

"Kila kitu kiko sawa!" Makombora yamerushwa kutoka Iran dhidi ya kambi mbili za jeshi zilizoko Iraq. Uchunguzi kuhusu hasara na uharibifu unaendelea. Hadi sasa kila kitu kiko sawa! "rais wa Marekani Donald Trump amebaini kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Kuuwawa kwa Soleimani Januari 3 kulizorotesha uhusiano kati ya Iran na Marekani.

Jenerali Soleimani - alikuwa kiongozi wa oparesheni ya kijeshi ya Iran katika eneo la mashariki ya kati - lakini serikali ya Marekani ilimuona kuwa gaidi, ambaye alihusika na vifo vya mamia ya wanajeshi wake na kwamba alikuwa akipanga shambulio "hatari".