MAREKANI-YEMENI-AQPA-USALAMA

Marekani yamuua Qassem al-Rimi, kiongozi wa kundi la Al-Qaeda katika rasi ya Arabia

Picha Qassem al-Rimi, mkuu wa kundi la Al-Qaeda katika rasi ya Arabia (Aqpa). Picha hii imetolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Yemeni.
Picha Qassem al-Rimi, mkuu wa kundi la Al-Qaeda katika rasi ya Arabia (Aqpa). Picha hii imetolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Yemeni. © AFP

Marekani imetangaza kwamba "imemuua" Qassem al-Rimi, kiongozi wa kundi la Al-Qaeda katika rasi ya Arabia (Aqpa) nchini Yemen, kundi la kijihadi ambalo lilidai kuhusika katika mashambulizi dhidi ya nchi za Magharibi.

Matangazo ya kibiashara

"Kwa maagizo ya rais Donald Trump, Marekani iliendesha operesheni ya kupambana na ugaidi nchini Yemen na ilifanikiwa kumuangamiza Qassem al-Rimi, mwanzilishi na kiongozi wa kundi la Al-Qaeda katika rasi ya Arabia (Aqpa)", ikulu ya White House imebaini katika taarifa.

Chini ya uongozi wa al-Rimi, Aqpa ilitekeleza "uhalifu mkubwa dhidi ya raia nchini Yemen na ilitaka kutekeleza na kuhamasisha mashambulizi kadhaa dhidi ya Marekani na vikosi vyetu," taarifa hiyo imeongeza.

Kifo cha Qassem al-Rimi "kinadhoofisha zaidi Aqpa na kundi la Al-Qaeda na hii itaondoa vitisho ambavyo makundi hayo yamekua yanatoa kwa usalama wa taifa letu," pia ikulu ya White House imesema.

Kulingana na serikali ya Marekani, al-Rimi alijiunga na Al-Qaeda katika miaka ya 1990, akifanya kazi nchini Afghanistan kwa niaba ya Osama bin Laden, aliyehusika na shambulio la Septemba 11, 2001 nchini Marekani.

Aqpa ilitumia fursa ya kujidhatiti nchini Yemen kutokana na kudhoofika kwa serikali kuu ya nchi hiyo Kusini na Kusini-Mashariki mwa nchi, inayoendelea kukumbwa na vita tangu mwezi Machi 2015.

Kundi la Al-Qaeda katika rasi ya Arabia (Aqpa) lilidai kuhusika katika shambulio la risasi lililotokea mwanzoni mwa mwezi Desemba katika kambi ya jeshi la Marekani huko Pensacola, Florida, lililoua askari wanamaji watatu, kwa mujibu wa taarifa ya Jumapili kutoka shirika la Marekani linalokaguwa tovuti za makundi ya wanamgambo wa Kiislam.