SYRIA-USALAMA-SIASA

Syria: Vikosi vya serikali vyasonga mbele katika ngome ya mwisho ya wanajihadi

Askari wa jeshi la Syria akitoa ulinzi karibu na bango linaloandikwa "Saraqeb" katika mji wa Tall Sultan katika Mkoa wa Idleb.
Askari wa jeshi la Syria akitoa ulinzi karibu na bango linaloandikwa "Saraqeb" katika mji wa Tall Sultan katika Mkoa wa Idleb. AFP

Vikosi vya serikali ya Syria vimesonga mbele Kaskazini Magharibi mwa Syria dhidi ya wanajihadi na waasi, na kuweka kwenye himaya yao kambi ya jeshi waliyopoteza kwa kipindi cha zaidi ya miaka saba iliyopita,shirika la haki za binadamu nchini Syria (OSDH) limeripoti.

Matangazo ya kibiashara

Wanajihadi wa kundi la Hayat Tahrir al-Cham (HTS, tawi la zamani la Al-Qaeda nchini Syria) wanadhibiti nusu ya Mkoa wa Idleb na pia baadhi ya maeneo ya Mikoa ya Aleppo, Hama na Latakia.

Makundi ya waasi na makundi mengine ya wanajihadi yenye ushawishi mdogo pia yapo katika maeneo hayo, ambayo ni ngome kubwa ya wanajihadi, ambapo serikali imeshindwa kudhibiti.

Katikati ya mwezi Desemba 2019, majeshi ya serikali ya Bashar al-Assad, yakisaidiwa na Urusi, walishambulia tena mkoa wa Idleb.

Baada ya "mapigano makali" kabla ya alfajiri dhidi ya wanajihadi na waasi, vikosi vya serikali vimedhibiti kambi ya 46, kilomita 12 magharibi mwa mji wakwanza kwa ukubwa wa Aleppo, shirika la Haki za Binadamu nchini Syria (OSDH) limebaini.

Vikosi vya Uturuki vilikuwa katika kambi hiyo lakini viliondoka Alhamisi, chanzo hicho kimesema.