MAREKANI-AFGHANISTANI-TALIBAN-USALAMA

Marekani yaendesha mashambulizi ya anga dhidi ya Taliban, mchakato wa amani hatarini

Marekani imefanya mashambulizi ya anga dhidi ya wapiganaji wa Taliban Jumatano hii Machi 4, katika jimbo la Helmand, Kusini mwa Afghanistan, msemaji wa vikosi vya Marekani ametangaza.

Machi 2, 2020, wapiganaji wa Taliban na wanakijiji wa Afghanistan walisherehekea mkataba uliofikiwa kati kundi hilo na Washington, katika wilaya ya Alingar (mkoa wa Laghman).
Machi 2, 2020, wapiganaji wa Taliban na wanakijiji wa Afghanistan walisherehekea mkataba uliofikiwa kati kundi hilo na Washington, katika wilaya ya Alingar (mkoa wa Laghman). NOORULLAH SHIRZADA / AFP
Matangazo ya kibiashara

Ni mashambulizi ya kwanza ya Marekani tangu Washington na Taliban kutia saini makubaliano ya kuondoka kwa vikosi vya nchi hiyo nchini Afhganistan siku ya Jumamosi wiki iliyopita.

Kanali Sonny Leggett, msemaji wa vikosi vya Marekani nchini Afghanistan, amethibitisha mashamulizi hayo kwenye ukurasa wake wa Twitter. Amesema wapiganaji wa Taliban "walishambulia kwa nguvu kizuizi cha barabara [cha vikosi vya usalama vya Afghanistan]. Mashambulizi tuliyotekeleza ni ya kujihami ili kukomesha shambulio hilo la taliban. "

Marekani inaendelea kuunga mkono mchakato wa amani, msemaji wa vikosi vya Marekani nchini Afghanistan ameongeza. amewaasihi wapiganaji wa Taliban kukomesha "mashambulizi yao ambayo hayana umuhimu wowote" na kuheshimu ahadi zao.

Mkataba uliyotiwa saini Jumamosi huko Doha, unaitaka Marekani kuondoa vikosi vyake ndani ya kipindi cha miezi 14 na serikali ya Kabul na Taliban kuanza mazungumzo.

Mashambulizi hayo ya kujihami ya Marekani yanajibu mashambulizi ya Taliban yaliyotokea usiku wa Jumanne kuamkia Jumatano. Karibu askari 20 wa Afghanistan na polisi waliuawa.