AFGHANISTAN-SIASA-USALAMA

Ashraf Ghani na Abdullah Abdullah wajitangaza kila mmoja rais wa Afghanistan

Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani (katikati), Makamu wa Kwanza wa rais Amrullah Saleh (kushoto) na Makamu wa Pili wa rais Sarwar Danish (kulia), katika sherehe yao ya kutawazwa mjini Kabul, Machi 9, 2020.
Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani (katikati), Makamu wa Kwanza wa rais Amrullah Saleh (kushoto) na Makamu wa Pili wa rais Sarwar Danish (kulia), katika sherehe yao ya kutawazwa mjini Kabul, Machi 9, 2020. REUTERS/Mohammad Ismail

Hali ya sintofahamu inaendelea nchini Afghanistan, baada ya siku chahe kufanyika uchaguzi nchini humo, ambapo rais Ashraf Ghani alidai alishinda, huku mpizani wake Abdullah Abdullah pia akidai alishinda.

Matangazo ya kibiashara

Rais Ashraf Ghani na mpinzani wake mkuu Abdullah Abdullah wote waliapishwa Jumatatu kama marais wa Afghanistan, hali ambayo inatumbukiza nchi hiyo katika mzozo mpya wa kitaasisi ambao utachelewesha kuanza kwa mazungumzo ya amani ya kipekee na Taliban.

Milipuko ilisikika wakati wa sherehe hizo huko Kabul: Kundi la Islamic State (IS) imedai kuwa wapiganaji wake walifyatua makombora kumi. Wizara ya Mambo ya Ndani inasema makombora manne ndio yalirushwa na afisa mmoja wa polisi alijeruhiwa kidogo.

Tukio hili linaonyesha kwamba usalama bado unalegalega licha ya mchakato wa amani ambao ulipelekea kutiwa saini kwenye mkataba wa kihistoria huko Doha kati ya Marekani na Taliban, tarehe 29 Februari, baada ya miaka 18 ya vita.

Wiki mbili zilizopita Marekani ilimtaka rais wa Afghanistan Ashraf Gahni kusogeza mbele sherehe ya kutawazwa kwake kwa muhula wa pili ili sherehe hiyo isihatarishi juhudi zake za amani nchini Afghanistan.

Ashraf Ghani alidai alishinda uchaguzi wa urais uliyofanyika Septemba 28, naye mpinzani wake, Abdullah Abdullah, pia alijitangaza mshindi wa uchaguzi huo.

Marekani mpaka sasa haijatambua mshindi wa uchaguzi wa urais nchini Afghanistan na hali hii inatishia mchakato wa amani, mchakato ambao unasimamiwa na Marekani.