Coronavirus: Muungano unaongozwa na Riyadh watangaza kusitisha mapigano Yemen
Imechapishwa:
Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, ambao unaendelea kupambana nchini Yemen kwa kusaidia vikosi vya serikali, umetangaza kusitisha mapigano kuanzia Alhamisi, Aprili 9 katika kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19, msemaji wa jeshi la Saudi Arabia, Kanali Turki al-Maliki.
"Tunatangaza kusitisha mapigano kuanzia (Alhamisi) kwa muda wa wiki mbili. Tunasubiri waasi wa Houthis kukubali. Tunaanda hali ya kupambana dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 nchini Yemen, msemaji wa jeshi la Saudi Arabia, Kanali Turki al-Maliki, huku akibaini kwamba upande wao hatua hiyo itaanza kutekelezwa Alhamisi Aprili 09 saa 09:00 saa za kimataifa (GMT).
Hatua hiyo imechukuliwa kuitikia wito uliotolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres wa kutaka mapigano katika nchi zinazo kabiliwa na migogoro duniani yasimamishwe katika juhudi za kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona.
Antonio Guterres ameunga mkono tangazo la Saudi Arabia, huku akisema hatua hiyo inaweza kusaidia kuendeleza juhudi za kuleta amani na kupambana na janga la maambukizi ya virusi vya Corona.
Hata hivyo muda mfupi tu baada ya Saudi Arabia kutoa tamko juu ya kusimamisha mapigano wakaazi wa mji unaopiganiwa wa Marib walisema kwamba mji wao ulishambuliwa kwa kombora linalotuhimiwa kuwa la waasi wa Kihouthi.
Watu zaidi ya laki moja wamepoteza maisha kutokana na mgogoro huo ambao pia umesababisha maafa makubwa kwa mamilioni ya watu kutokana na uhaba wa chakula na huduma za afya.