SYRIA-USALAMA

Syria yakanusha ripoti ya OPCW ikishutumu kufanya mashambulizi ya kemikali

Serikali ya Syria imeendelea kunyooshewa kidole cha lawama kwa kufanya mashambulizi ya kemikali dhidi ya ngome za waasi.
Serikali ya Syria imeendelea kunyooshewa kidole cha lawama kwa kufanya mashambulizi ya kemikali dhidi ya ngome za waasi. Muhammad HAJ KADOUR / AFP

Utawala wa Damascus umefutilia mbali ripoti ya Shirika linalopiga marufuku silaha za Kemikali (OPCW) kwamba ndege za vikosi vya Syria ziliendesha mfululizo wa mashambulizi ya kemikali katika mji unaodhibitiwa na waasi, kwa agizo kutoka uongozi wa juu wa kijeshi nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Katika ripoti iliyotolewa Jumatano wiki hii, OPCW inasema vitengo vya jeshi la Syria vilifanya mashambulizi matatu ya kemikali magharibi mwa nchi hiyo mnamo mwezi Machi 2017.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imesema katika taarifa kwamba ripoti ya OPCW ni ya" uongo na sio sahihi, ambayo lengo lake ni kupotosha ukweli na kuishtumu serikali ya Syria.

Hapo awali, Rais wa Syria Bashar al Assad na Urusi, ambayo inasaidia kijeshi Damascus, walirejelea kauli hiyo kwamba hawajawahi kutumia silaha za kemikali, wakiwatuhumu waasi wa Syria kwa kufanya mashambulizi ya kemikali ili kuvihusisha vikosi vya serikali.