PAKISTANI-RAMADHAN-CORONA-AFYA

Coronavirus/Ramadhan: Madaktari nchini Pakistan waonya kuhusu kuongezeka kwa maambukizi zaidi

Mamlaka nchini Pakistani imewataka raia kuheshimu hatua ya kiusalama ya kutokaribiana wakati wa  swala misikitini.
Mamlaka nchini Pakistani imewataka raia kuheshimu hatua ya kiusalama ya kutokaribiana wakati wa swala misikitini. REUTERS/Akhtar Soomro

Wakati mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani unaanza Ijumaa hii, Aprili 24 kwa Waislamu wengi ulimwenguni, viongozi katika nchi kadhaa wameendelea kushikilia hatua ya kufunga misikiti kuzuia mikusanyiko ya watu kwa kukabiliana na kuenea kwa virusi vya Corona.

Matangazo ya kibiashara

Nchini Pakistan, mamlaka imeamua kuachia wazi misikiti kwa kuwaruhusu waumuini kuendelea kufanya ibada mbalimbali katika maeneo hayo ya ibada kwa Waislamu.

Hata hivyo madaktari wa Pakistan wametoa wito kwa serikali yao kurejelea uamuzi wake.

Madaktari wameonya kuwa maambukizi ya virusi vya Corona yanaweza kuongezeka katika mwezi huu wa Ramadhan kutokana na hatua ya serikali kuamua kufungua misikiti na kuruhusu mamia ya Waislamu kushirika ibada katika shemu hizo takatifu kwa Waislamu.

Katika mkutano na waandishi wa habari, madaktari wa Pakistan wamekosoa hatua ya serikali ya kuruhusu swala kufanyika katika misikiti, ambapo mamia kwa maelfu ya waumini wanatarajia kushiriki katika mwezi huu mtukufu.

Mamlaka nchini Pakistani imwataka waumini wa Kiislamu kuheshimu hatua ya kutokaribiana iliyotolewa na serikali wakati wa swala misikitini, huku ikiwataka wazee na watu ambao afya zao sio nzuri kubaki nyumbani.

Hata hivyo madaktari wamesema hatua hizo hazitoshi, huku wakiwanyooshea kidole cha lawama viongozi wa Pakistan na viongozi wa kidini nchini humo.

Janga la Covid-19 limeua watu zaidi ya 200 nchini Pakistan, nchi ya pili kwa Waislamu wengi duniani, huku kukiripotiwa visa 10,500vya maambukizi.