YEMEN-UN-CORONA-AFYA-UCHUMI

Umoja wa Mataifa: Watu milioni moja wako katika hatari ya kupata virusi vya Corona Yemen

Hali ya sintofahamu yaendelea kuikumba Yemen.
Hali ya sintofahamu yaendelea kuikumba Yemen. MOHAMMED HUWAIS / AFP

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa zaidi ya watu milioni moja nchini Yemen ambao hawana makao rasmi wako katika hatari ya kupoteza makazi yao, pamoja na kupata virusi vya Corona ambayo vinasambaa kwa kasi katika taifa hilo.

Matangazo ya kibiashara

Umoja wa Mataifa umesema dola Millioni 89.4 zinahitajika kuwasadia wakimbizi nchini Yemen kupambana na virusi vya Corona.

Ripoti iliyotolewa na kituo cha kimataifa kinachofuatilia watu wanaoyakimbia maskani yao, IDMC, imesema mwaka 2019 hali mbaya ya hewa iliwalazimisha kiasi watu milioni 24 kote duniani kuhama kutoka maeneo waliyokuwa wakiishi.

Watu wengine karibu milioni 9.5 walilazimika kuchukua hatua kama hiyo kutokana na masuala mengine, vikiwemo vita.

Kulingana na ripoti ya IDMC, karibu watu milioni 51 wamepoteza makaazi na wengi wanaishi kwenye kambi zenye mifumo dhaifu ya usafi na sasa wanazongwa na kadhia ya janga la virusi vya Corona.

Mamilioni ya watu walikimbia mafuriko, vimbunga, moto wa nyika, ukame, maporomoko ya udongo, matetemeko ya ardhi na hali mbaya ya hewa kama joto lililopindukia viwango vya wastani.

Ripoti hiyo imeorodhesha masuala kama ukosefu wa maji, sabuni na vifaa vingine vya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 kuwa kitisho cha wazi katika makambi au makaazi duni yanayohifadhi watu hivi sasa.