IRAN-USALAMA

Askari 19 wa kikosi cha wanamaji wa Iran wauawa katika Ghuba

Picha iliyotolewa Desemba 27, 2019 na televisheni ya serikali ya Iran IRIB, ikionyesha meli ya Jamaran wakati wa mazoezi ya kijeshi ya majini ya Irani, Urusi na China katika Bahari ya Hindi na Bahari ya Arabia.
Picha iliyotolewa Desemba 27, 2019 na televisheni ya serikali ya Iran IRIB, ikionyesha meli ya Jamaran wakati wa mazoezi ya kijeshi ya majini ya Irani, Urusi na China katika Bahari ya Hindi na Bahari ya Arabia. © AFP

Meli ya kivita ya Iran imepigwa kombora wakati wa mazoezi ya kijeshi ya baharini katika Bahari ya Arabia, na kusababisha vifo vya askari 19 wa kikosi cha wanamaji wa nchi hiyo. Hali hii inatokea wakati huu ambapo mvutano unaendelea kati ya nchi hiyo na Marekani katika maji ya Ghuba.

Matangazo ya kibiashara

Ajali hiyo ilitokea Jumapili alasiri karibu na mkoa wa Bandar-e Jask, kwenye pwani ya Kusini mwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, televisheni ya serikali ya iran imesema leo Jumatatu kwene mtandao wake.

Katika taarifa, jeshi la Iran limesema askari 19 waliuawa na 15 walijeruhiwa katika "ajali" hilo iliyohusisha chombo cha usaidizi wa vifaa cha Konarak wakati wa mazoezi, bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi.

Meli hiyo imesafirishwa kwa "uchunguzi wa kiufundi," taarifa hiyo imeongezea, huku ikitoa wito wa "kuepuka uvumi" hadi habari zaidi zitakapotolewa.

Shirika la habari la Iran, Tasnim, limesema katika ukurasa wake wa twitter kwa Kiingereza kuwa "Konarak imepigwa kombora kutoka kwa meli nyingine ya rafiki, ya Jamaran, huku likibaini kwamba ni tukio lililotokea kwa bahati mbaya.