AFGHANISTANI-USALAMA

Afganistani: Saba waangamia katika shambulizi la kujitoa mhanga

Wanajeshi wa Afghanistan katika eneo la shambulio la kujitoa mhanga huko Kabul, Aprili 29, 2020.
Wanajeshi wa Afghanistan katika eneo la shambulio la kujitoa mhanga huko Kabul, Aprili 29, 2020. REUTERS/Omar Sobhani

Watu wasiopungua saba wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulizi la kujitoa mhanga lililotokea leo Jumatatu katika eneo la Ghazni Mashariki mwa Afghanistan, maafisa wameliambia shirika la habari la AFP. Kundi la Taliban limekiri kuhusika na shambulio hilo.

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na msemaji wa gavana wa Mkoa wa Ghazni, Wahidullah Jumazada, shambulio hilo, lilitekelezwa kwa bomu lililotegwa ndani ya gari la jeshi na lilikuwa limelenga jengo la idara ya ujasusi la Afghanistan. Watu 7 wameuawa na 40 kujeruhiwa.

Wote waliopoteza maisha ni maafisa wa idara ya ujasusi, amesema Wahidullah Jumazada, huku akibaini kwamba hakuna raia wowote aliyejeruhiwa.

Mkurugenzi wa hospitali ya Ghazni, Baz Mohammad Himmat, amebaini kwamba watu 7 wameuawa na 25 wamejeruhiwa.

Kundi la Taliban limekiri kuhusika na shambulizi hilo, lililotekelezwa kwa mujibu wa Zabihullah Mudjahid na mshambuliaji wa kujitoa mhanga "katika kujibu tangazo la vita lililotolewa na adui."

Afghanistan inakabiliwa ongezeko la machafuko, licha ya mkataba uliofikiwa mwishoni mwa mwezi Februari kati Taliban na Marekani, mkataba ambao unatoa nafasi kwa majeshi ya kigeni kuondoka nchini humo ifikapo katikati ya mwaka 2021.

Serikali iliamuru vikosi vya usalama "kuanza tena shughuli zao (mashambulizi) dhidi ya adui", zilizokuwa zimesitishwa tangu Marekani na Taliban kufikia mkataba huko Doha, baada ya shambulio la Jumanne dhidi ya hospitali ya wazazi huko Kabul lililogharimu maisha ya watu 24.