ISRAELI-SIASA

Israel: Serikali mpya ya Netanyahu-Gantz yakula kiapo mbele ya Bunge

Benjamin Netanyahu na Benny Gantz wameunda serikali ya mseto, Mei 17, 2020.
Benjamin Netanyahu na Benny Gantz wameunda serikali ya mseto, Mei 17, 2020. RONEN ZVULUN, Jack GUEZ / AFP

Baada ya siku 500 za mgogoro na chaguzi tatu bila ushindi wa wa viti vingi bungeni kati ya Benjamin Netanyahu na Benny Gantz, hatimaye Bunge la Israeli limetoa baraka zake kwa serikali mpya ya umoja.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii sasa inamaliza mgogoro wa muda mrefu zaidi wa kisiasa katika historia ya taifa la Israel.

Wabunge waliidhinisha serikali hiyo itakayoongozwa kwa miaka mitatu kwa kura 73 dhidi ya 46 za waliopinga na mbunge mmoja hakuhudhuria. Bunge la Israel lina viti 120.

Serikali hiyo mpya inayoingia baada ya siku 500 za kutokuwepo na serikali thabiti imejiandaa kukabiliana na mizozo mikubwa katika wiki zake za mwanzo ikiwa ni pamoja na kuanguka kwa uchumi kulikosababishwa na janga la virusi vya Corona.

Waziri mkuu Benjamin Netenyahu anatarajiwa kuongoza kwa miezi 18 kabla ya mpinzani wake mkuu Benny Gantz kuchukuwa hatamu za uongozi,kwa mjibu wa makubaliano yao.

Netanyahu na Gantz , mkuu wa zamani wa jeshi, wametangaza mwezi uliopita wataweka kando tofauti zao na uadui na kujiunga pamoja kuielekeza nchi hiyo kupitia katika mzozo wa virusi vya corona pamoja na hali mbaya ya kiuchumi.

Makubaliano hayo hata hivyo, yamesababisha kusambaratika kwa chama cha Gantz cha Bluu na Nyeupe, na kuvunja ahadi yake ya kampeni ya kutohudumu chini ya Netanyahu, anaesubiri kupandishwa kizimbani kwa mashtaka ya rushwa.