Watoto wa Khashoggi 'wasamehe' wauaji wa baba yao
Imechapishwa:
Watoto wa mwandishi wa habari wa Saudia Jamal Khashoggi, aliyeuawa mnamo mwezi Oktoba 2018 kwenye ubalozi wa Saudi Arabia katika mji mkuu wa Uturuki, Istanbul, wamesema leo Ijumaa kuwa wamewasamehe wauaji wa baba yao.
"Wakati wa usiku huu mtakatifu wa mwezi huu mtakatifu (wa Ramadhani) tunakumbuka maneno ya Mwenyezi Mungu aliposema: ikiwa mtu anasamehe na akakubali kupatanishwa, mtu huyo ana ujira mkubwa mbele yake Mwenyezi Mungu," Salah Khashoggi, mtoto wa mwandishi huyo wa habari, ameandika kwenye Twitter.
"Hii ndio sababu sisi, watoto wa marehemu Jamal Khashoggi, tunatangaza kwamba tumewasamehe wale waliomuua baba yetu," ameongeza.
Jamal Khashoggi aliuawa Oktoba 2, 2018 katika majengo ya ubalozi wa Saudi Arabia huko Istanbul. Washtakiwa watano walihukumiwa kifo na wengine watatu kufungwa jela baada ya kesi iliyosikilizwa Desemba mwaka jana nchini Suadi Arabia.