AFGHANISTANI-TALIBAN-USALAMA

Afganistani: Wanamgambo 900 wa Taliban waachiwa huru

Wafungwa wa Taliban waliokuwa wanazuiliwa katika jela la Bagram wameachiwa huru, kilomita 50 kutoka Kabul, Mei 26, 2020.
Wafungwa wa Taliban waliokuwa wanazuiliwa katika jela la Bagram wameachiwa huru, kilomita 50 kutoka Kabul, Mei 26, 2020. WAKIL KOHSAR / AFP

Serikali ya Kabul inatarajia kuongezwa muda wa usitishwaji mapigano, baada ya wanamgambo 900 wa kundi la Taliban kuachiwa huru Jumanne wiki hii kwa jumla ya wanamgambo 2000 ambao rais Ashraf Ghani alitangaza kwamba atawaachia huru hivi karibuni.

Matangazo ya kibiashara

Mwishoni mwa wiki iliyopita kundi la Taliban lilitangaza kusitisha mapigano kwa muda wa saa 72 kutokana na kusherehekea siku kuu ya Eid el Fitri, hatua ambayo iliungwa mkono na kukubaliwa na serikali ta Afghanistan.

Wapiganaji hao 900 walikuwa wanazuiliwa katika jela za Pol-e-Charkhi na Bagram huko Kabul, na vile vile katika jela za mikoa mingine 19. Ukombozi ulianza saa sita mchana na kumalizika jioni.

Wafungwa hao 900 wa kundi la Taliban wanakuja kujiongeza kwenye idadi ya wafungwa wengine 1,000 waliochiliwa huru kabla ya hatua ya kundi hilo kusitisha mapigano mapema wiki iliyopita, na kufanya idadi ya wafungwa 2000 wa kundi hilo ambao sasa wameachiliwa huru.

Wafungwa hao 900 ni kundi kubwa la wafungwa kuachwa huru tangu Marekani na kundi la Taliban walipotia saini makubaliano ya amani mapema mwaka huu ambayo yameelezea kuhusu kubadilishana wafungwa kati ya pande hizo zilizomo vitani.

Kuna matarajio kuwa hatua hiyo ya kuwaacha huru wafungwa inaweza kusababisha kupungua kwa ghasia , na maafisa wa Taliban wanasema wanatafakari kurefusha muda huo wa kusitisha mapigano. Kuachiwa huru kwa wafungwa ni sehemu ya makubaliano kati ya Marekani na Taliban, yaliyotiwa saini Februari 29 kuruhusu majeshi ya Marekani na yale ya NATO kuondolewa nchini humo.