IRAN-MAREKANI-USALAMA-HAKI

Raia wa Iran aliyehukumiwa kwa kifo cha Soleimani kunyongwa

Kiongozi Mkuu wa Irani Ayatollah Ali Khamenei na Rais wa Irani Hassan Rouhani wakisalia maiti ya Meja-Jenerali Qassem Soleimani, mkuu wa kikosi cha Quds, ambaye aliuawa katika shambulio la anga la ndege ya Marekani kwenye uwanja wa ndege wa Baghdad, Tehran
Kiongozi Mkuu wa Irani Ayatollah Ali Khamenei na Rais wa Irani Hassan Rouhani wakisalia maiti ya Meja-Jenerali Qassem Soleimani, mkuu wa kikosi cha Quds, ambaye aliuawa katika shambulio la anga la ndege ya Marekani kwenye uwanja wa ndege wa Baghdad, Tehran ©Official President's website/Handout via REUTERS

Raia wa Iran aliyehukumiwa kwa kutoa habari iliyosababisha kuuawa kwa Mkuu wa kikosi cha Irani Qassem Soleimani atauawa hivi karibuni, mahakama ya Iran imetangaza leo Jumanne.

Matangazo ya kibiashara

Meja Jenerali Qasem Soleimani, aliye kuwa mkuu wa vikosi vya kikurdi nchini Iran- kitengo maalum cha jeshi la Iran (Revolutionary Guards) ambacho huendesha opareshani zake nje ya nchi, aliuawa Januari 3, 2020 nchini iraq katika shambulizi la anga la ndege isiyokuwa na rubani ya Marekani.

"Mahmoud Mousavi-Majd, mmoja wa watu waliotumiwa na idara ya ujasusi ya Marekani ya CIA na Mossad, Idara ya ujasusi ya Israel, alihukumiwa kifo. Aliwapatia maadui zetu habari kuhusu shujaa Soleimani," amesema Gholamhossein Esmaili, msemaji wa mahakama nchini Irani, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliorushwa hewani kwenye televisheni.

Kifo cha Jenerali Soleimani kilizusha mvutano mkubwa kati ya Marekani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Siku chache baada ya tukio hilo, Iran ilizindua mashambulizi kadhaa ya kulipiza kisasi. Katika mashambuliei hayo ndege ya shirika la Ukraine ilijikuta ilishambuliwa kimakosa na kusababisha vifo vya abiria 176 ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa ndege hiyo.

Meja Jenerali Qasem Soleimani alikuwa kiungo muhimu katika mapambano ya kimkakati mashariki ya kati kupitia vikosi vya Kikurdi, ambavyo vinaendesha oparesheni yake kwa ushirikiano na jeshi la ulinzi la Iran.

Jina lake lilianza kuwa maarufu alipopewa nafasi ya kuongoza kikosi cha Quds na kujenga ushirikiano wa karibu na kiongozi mkuu wa kidini Ayatollah Khamenei kiasi wakati mmoja ulamaa huyo alishiriki na kufungua dhifa ya harusi ya binti ya Jenerali Soleimani.

Meja jenerali Qasem Soleimani, na vikosi vyake vinafanya kazi chini ya kiongozi mkuu wa kidini, Ayatollah Ali Khamanei, badala ya kufuata muundo wa kawaida wa kijeshi wa Iran.

Jenerali Qasem Soleimani hakuwa anajulikana na wengi nchini Iran hadi mwaka 2003 wakati Marekani ilipoivamia kijeshi Iraq.

Umashuhuri wake uliimarika hatua ambayo ilifanya maafisa kadhaa wa Marekani kutoa wito wa kuuliwa kwake.

Muongo mmoja na nusu baadae Soleimani alifikia kuwa kamanda maarufu wa vita nchini Iran kiasi akipuuza miito ya umma kumtaka aingie kwenye siasa.