AFGHANISTANI-TALIBAN-USALAMA

Afghanistan: Shambulio jipya dhidi ya msikiti laua watu wanne Kabul

Lango la msikiti wa Sher Shah Suri unaolindwa na maafisa wa polisi, Juni 12, 2020 huko Kabul.
Lango la msikiti wa Sher Shah Suri unaolindwa na maafisa wa polisi, Juni 12, 2020 huko Kabul. STR / AFP

Watu wasiopungua wanne wameuawa leo Ijumaa katika shambulio lililotekelezwa dhidi ya Msikiti katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul, ikiwa ni shambulio la pili katika kipindi kisichozidi wiki mbili.

Matangazo ya kibiashara

"Kulingana na habari zetu za awali, vilipuzi vilivyowekwa ndani ya msikiti huo vimelipuka wakati wa sala ya Ijumaa," Tariq Arian, msemaji wa wizara ya usalama amesema katika ujumbe mfupi uliotumwa kwa shirika la habari la AFP kupitia WhatsApp.

Imam aliyekuwa akiongoza sala hiyo na waumini watatu wameuawa na wengine wanane kujeruhiwa, msemaji huyo ameongeza. Wizara ya Afya imethibitisha idadi ya vifo hivyo vinne.

Shambulio hilo, ambalo ni la pili dhidi ya msikiti huko Kabul katika kipindi kisichozidi wiki mbili, bado halijadaiwa na kundi lolote.

Juni 3, Imam mwengine aliyefahalika kwa hotuba zake zenye utata aliuawa na muumini mmoja katika msikiti unaopatikana katika eneo la Green Zone, eneo la katikati mwa mji wa Kabul. Kundi la Islamic State lilikiri kuhusika na shambulio hilo.

Misikiti hulengwa mara kwa mara nchini Afghanistan. Mwezi Oktoba mwaka jana, waumini 62 waliuawa na zaidi ya 30 walijeruhiwa katika shambulio lililotokea katika msikiti huko Nangarhar, Mashariki mwa Afghanistan.

Machafuko yamepungua nchini Afghanistan tangu Mei 24, wakati kundi la Taliban lilipotangaza kusitisha mapigano kwa muda wa siku tatu kutokana na sherehe ya Eid. Hata hivyo mpango huo haukudumu, licha ya maombi kadhaa kutoka kwa serikali ya Afghanistan, na lilianzisha tena mashambulio dhidi ya vikosi vyake vya usalama.