IRAN-USALAMA

Iran: Kituo cha kuzalisha nguvu za nyuklia cha Natanz chaharibiwa kwa moto

Kituo cha kurutubisha madini ya urani cha Natanz kimeharibiwa vibaya kwa moto.
Kituo cha kurutubisha madini ya urani cha Natanz kimeharibiwa vibaya kwa moto. Reuters

Maafisa nchini Iran wanasema moto mkubwa uliozuka siku ya Jumanne kwenya kiwanda cha kuzalisha nguvu za  nyuklia  umesababisha madhara makubwa.

Matangazo ya kibiashara

Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, AEOI, limesema kuwa kituo chake cha kurutubisha madini ya urani cha Natanz kimeharibiwa vibaya kwa moto.

Aidha wanasema marekebisho yanafanyika  kubadilisha mashine zilizoharibika na mashine zenye uwezo mkubwa zaidi  , huku ikishtumu maadui wa nhi hiyo kushambulia kituo hicho katika eno la Natanz.

Hata hivyo, Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran limesema hakukuwa na vifaa vyovyote vya nyuklia katika kituo cha Natanz ambacho sehemu yake kubwa iko chini ya ardhi. 

Msemaji wa shirika hilo, Behrus Kamalvandi ameliambia shirika la habari la Iran, IRNA kwamba tukio hilo huenda likachelewesha maendeleo ya urutubishaji wa madini ya urani kwa muda, lakini serikali ya Iran itakikarabati kituo hicho kwa kujenga jengo kubwa lenye vifaa vya kisasa zaidi.

Baadhi ya maafisa wanahofia kwamba huenda mataifa adui wa Iran kama vile Marekani na Israel yanahusika na tukio hilo, lakini hakuna ushahidi au uthibitisho ambao umetolewa. Katika siku za nyuma, kirusi cha kwenye komyputa cha Stuxnet kilitumika kukivamia kituo cha nyuklia cha Natanz. Iliaminika kwa kiasi kikubwa kwamba Marekani na Israel ndiyo walikitengeza kirusi hicho.

Hivi karibuni, shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Nishati ya Nyuklia, IAEA liliishinikiza Iran kuruhusu ukaguzi wa nyuklia kwenye vinu vyake vya nyuklia vyenye utata. Kituo cha Natanz kimekuwa kikifuatiliwa na IAEA.