SAUDI ARABIA-HIJA-CORONA-AFYA

Ibada ya kila mwaka ya Hija yaanza Makka

Ibada kubwa ya Hija inayotekelezwa kila mwaka na waumini wa Kislamu walio nauwezo inaanza leo katika mji mtakatifu wa Makka, nchini Saudi Arabia chini ya kiwingu cha Covid-19.

Sehemu inayozunguka Kaaba imeandaliwa kuwapokea mahujaji, Jumatatu, Julai 27.
Sehemu inayozunguka Kaaba imeandaliwa kuwapokea mahujaji, Jumatatu, Julai 27. Saudi Ministry of Media via AP
Matangazo ya kibiashara

Mwaka huu ibada hii ya Hija itashuhudia idadi ndogo kabisa ya mahujaji katika historia kutokana na janga Covid-19 ambalo limeendelea kusambaa katika nchi mbalimbali duniani.

Waaumini tu wanaoishi nchini Saudi Arabia watahudhuria ibada hiyo mwaka huu, ikiwa ni pamoja na 70% ya raia wa kigeni waishio nchini Saudi Arabia na 30% ya wananchi wa nchi hiyo.

Wakati huo huo serikali imesema kuna uwakilishi wa mataifa 160 ambayo kwa kawaida waumini wake wa kiislamu kila mwaka hushiriki ibada hiyo.

Saudi Arabia ndio nchi ya Ghuba ya Kiarabu iliyoathiriwa zaidi na janga la Covid-19.

Mwaka jana tu, waumini waKiislamu milioni 2.5, wengi wao kutoka nchi za kigeni, walishiriki katika ibada kubwa ya Hija kubwa huko Makka.

Hija, moja ya nguzo tano za dini ya Kiislamu na ambayo muumuni mwenye uwezo anapaswa kuitimiza walau mara moja katika maisha yake kwa kawaida ni moja ya mikusanyiko mikubwa sana ya kidini ulimwenguni.

Hata hivyo mlipuko wa janga la Covid-19 umeilazimisha Saudi Arabia kuzuia safari za mamilioni ya waumini, na mahujaji wachache waliochaguliwa wamepimwa virusi vya Corona na kwa siku kadhaa waliwekwa karantini katika hoteli mjini Makka.

Mahujaji wote watatakiwa kuvaa barakoa na kuzingtia kanuni za kujitenga katika mfululizo wa ibada zitakazofanyika katika mji mtukufu wa Makka na maeneo jirani ya magharibi ya Saudi Arabia.