IRAN-LEBANON-USALAMA-MSAADA

Iran yapendekeza msaada kwa Lebanon baada ya milipuko huko Beirut

Rais wa Iran Hassan Rohani.
Rais wa Iran Hassan Rohani. © AFP

Rais wa Iran amependekeza kupeleka msaada wa matibabu nchini Lebanon baada ya milipuko miwili katika bandari ya Beirut ambayo iliyosababisha vivo vya zaidi ya watu 100 na karibu 4,000 kujeruhiwa.

Matangazo ya kibiashara

"Iran inatangaza kuwa iko tayari kutuma msaada wa matibabu nchini Lebanon na pia inapendekeza kutoa huduma kwa wagonjwa waliojeruhiwa na msaada wowote wa matibabu unaohitajika," Hassan Rouhani amesema, kulingana na runinga ya serikali.

"Tunatumai kuwa kiini cha milipuko hiyo kitajulikana haraka iwezekanavyo na kwamba amani itarejea kwa mji wa Beirut," ameongeza.

Ripoti zinasema kuwa hospitali katika jiji hilo zimejaa majeruhi wanoahitaji msaada mkubwa, katika kipindi hiki ambacho nchi hiyo pia inaendelea kukabiliwa na virusi vya Corona.

Hakuna ripoti kamili kuhusu kilichotokea lakini, Wizara ya Mambo ya ndani inasema kuwa jengo ambalo milipuko hiyo ilitokea ilikuwa inahifadhi kemikali aina ya ammonium Nitrate kwa miaka sita.

Serikali nchini humo imetangaza hali ya hatari na maombolezo ya kitaifa kwa muda wa siku tatu.

Maafisa wa serikali hawakusema kipi hasa kilisababisha moto uliochochea miripuko hiyo, lakini chanzo kimoja cha usalama na vyombo vya habari vya Beirut vilisema cheche za moto zilitokana na wafanyakazi wa kuchomelea vyuma waliokuwa wakiziba tundu kwenye ghala hilo.

Nalo Baraza la jeshi nchini humo limetangaza kuwa limeanza kuchunguza kiini cha milipuko hiyo.

Iran inaunga mkono Hezbollah, chama cha kisiasa na kundi la Kishia lenye silaha ambalo lina ushawishi mkubwa nchini Lebanon.