LEBANON-USALAMA

Lebanon yaomboleza vifo vya watu 100

Rasi Michel Aoun alisema kwamba tani 2,750 za ammonium nitrate zilikuwa zimewekwa vibaya katika ghala moja kwa miaka sita.
Rasi Michel Aoun alisema kwamba tani 2,750 za ammonium nitrate zilikuwa zimewekwa vibaya katika ghala moja kwa miaka sita. AP Photo/Hassan Ammar

Nchi ya Lebanon ipo kwenye maombolezo baada ya watu 100 kupoteza maisha na wengine zaidi ya Elfu nne kujeruhiwa baada ya kutokea mlipuko mkubwa jijini Beirut.

Matangazo ya kibiashara

Mashambulio mawili katika bandari ya Beirut , yalitetikisa jiji lote na kusababisha moto mkubwa katika eneo hilo.

Ripoti zinasema kuwa hospitali katika jiji hilo zimejaa majeruhi wanoahitaji msaada mkubwa, katika kipindi hiki ambacho nchi hiyo pia inaendelea kukabiliwa na virusi vya Corona.

Hakuna ripoti kamili kuhusu kilichotokea lakini, Wizara ya Mambo ya ndani inasema kuwa jengo ambalo milipuko hiyo ilitokea ilikuwa inahifadhi kemikali aina ya ammonium Nitrate kwa miaka sita.

Serikali nchini humo imetangaza hali ya hatari na maombolezo ya kitaifa kwa muda wa siku tatu.

Maafisa wa serikali hawakusema kipi hasa kilisababisha moto uliochochea miripuko hiyo, lakini chanzo kimoja cha usalama na vyombo vya habari vya Beirut vilisema cheche za moto zilitokana na wafanyakazi wa kuchomelea vyuma waliokuwa wakiziba tundu kwenye ghala hilo.

Nalo Baraza la jeshi nchini humo limetangaza kuwa limeanza kuchunguza kiini cha milipuko hiyo.

Mataifa mbambali kama Ufaransa, Uingereza, Israel na mengine, yamesema kuwa yanatoa msaada kwa taifa hilo, huku rais Donald Trump akisema huenda kilichotokea kinaonekana ni shambulizi la bomu kwa tathmini ya Majenerali wa kijeshi waliozungumza naye.

Janga hili limetokea wakati nchi hiyo inapoendelea kupitia kipindi kigumu cha kiuchumi, lakini pia wanananchi wa taifa hilo wakisubiri uamuzi wa Mahakama siku ya Ijumaa kuhusu kuuawa kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Rafik Hariri mwaka 2005.