LEBANON-UCHUNGUZI-USALAMA

Uchunguzi waanzishwa kubaini kiini cha milipuko miwili mikubwa Beirut

Agosti 6, 2020: bandari ya Beirut iliharibiwa na milipuko ya Agosti 4.
Agosti 6, 2020: bandari ya Beirut iliharibiwa na milipuko ya Agosti 4. REUTERS/Issam Abdallah

Maafisa nchini Lebanon wameanza kuchunguza kiini cha milipuko miwili mikubwa iliyotokea jiini Beirut na kusababisha vifo vya watu 135 na kuwajeruhi wengine 5,000 wakati huu mataifa mbalimbali duniani yanapoendelea kujitokeza kulisaidia taifa hilo.

Matangazo ya kibiashara

Wachunguzi hao wanatathmini iwapo utunzaji wa kemikali aina ya ammonium nitrate, inayoaminika kusababisha milipuko hiyo mikubwa, ilifanyika kwa makusudi.

Mpaka sasa haijathibitishwa kiini hasa cha milipuko hiyo lakini maafisa nchini humo wanashuku kuwa, kuwepo kwa tani zaidi ya Elfu mbili na Mia Saba ndio chanzo cha janga hilo.

Baadhi ya wafanyakazi wa Bandari, waliohusika na utunzaji wa kemikali hiyo kwa sasa wamezuiwa majumbani mwao wakati huu,  Baraza la jeshi likionya kuwa litawachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kuhusika.

Idadi na vifo inatarajiwa kuongezeka, huku uongozi wa jiji la Beirut ukisema watu zaidi ya Laki Tatu, hawana makazi.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anakwenda nchini Lebanon leo, kuonesha masikitiko ya nchi yake kuhusu tukio hili, wakati huu nchi hiyo ikisema itawasaidia wananchi wa taifa hilo.

Shirika la Amnesty International, linataka kufanyika kwa ucunguzi wa kimataifa kubaini ukweli kuhusu milipuko hiyo.