ISRAELI-UAE-USHIRIKIANO

Umoja wa Falme za Kiarabu na Israeli wafikia mkataba wa amani

Mwanamfalme Mohammed bin Zayed, hapa akizuru Amman, Jordan, mwaka 2018.
Mwanamfalme Mohammed bin Zayed, hapa akizuru Amman, Jordan, mwaka 2018. REUTERS/Muhammad Hamed

Israeli na Umoja wa Falme za Karabu zimefikia mkataba wa amani na kurejesha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili. Tangazo hilo limetolewa na Marekani, na kubaini kwamba ni mkataba wa amani 'wa kihistoria' kati ya 'marafiki wawili wakubwa' wa Marekani.

Matangazo ya kibiashara

Mkataba huu na hatua ya kufufua uhusiano kati ya mataifa haya mawili utakuwa wa kwanza kati ya Israeli na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Taarifa hiyo ya Marekani inasema kwamba nchi hizo mbili zimepanga kufungua balozi zao na kwamba katika siku chache zijazo watasaini mikataba kadhaa katika nyanja za usalama, nishati, mawasiliano, afya, usafiri wa anga (kwa matarajio ya usafiri wa ndege za moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili), mazingira ya utalii na hata utamaduni.

Taarifa hiyo pia imeelezea ushirikiano wa haraka kati ya Israeli na Umoja wa Falme za Kiarabu katika nyanja ya utafiti katika matibabu na chanjo dhidi ya ugonjwa hatari wa Corona.

Kulingana na taarifa kutoka Marekani, katika sehemu ya mpango huu, Israeli "inasitisha" mpango wake wa kuzifanya kuwa makazi ya Kiyahudi maeneo ya ukanda wa magharibi yanayokaliwa na Wapalestina.

Lakini kulingana na Waziri Mkuu wa Israeli Benyamin Netanyahu mpango huo "umeahirishwa" tu. Kulingana na Umoja wa Falme za Kiarabu, Israeli imesitisha kabisa mpango huo, hatua ambayo inaweza kudhaniwa kama ushindi wa kidiplomasia kwa niaba ya maslahi ya Palestina na ya nchi za Kiarabu.