LEBANON-SIASA-USALAMA

Lebanon kumteua waziri mkuu kabla ya kuwasili kwa Macron

Eneo lililoharibiwa kufuatia mlipuko huko Beirut mnamo Agosti 11, 2020.
Eneo lililoharibiwa kufuatia mlipuko huko Beirut mnamo Agosti 11, 2020. REUTERS/Thaier Al-Sudani

Wanasiasa nchini Lebanon wanatarajia kukubaliana juu ya uteuzi wa waziri mkuu mpya, ambaye inasadikiwa kuwa anaweza kuwa balozi wa Ujerumani Moustapha Adib, chini ya shinikizo kutoka kwa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anayetarajiwa kuzuru nchi hiyo Jumatatu jioni.

Matangazo ya kibiashara

Macron, ambaye hii ni ziara yake ya pili huko Lebanon tangu kutokea kwa mlipuko mkubwa uliosababisha vifo vingi katika bandari ya Beirut Agosti 4, aliwataka viongozi wa Lebanon kuunda mara moja "serikali inayowajibika" ili kuiondoa nchi hiyo katika mgogoro wa kiuchumi na kisiasa.

Wengi wa wabunge, ambao wamekuwa wakikutana kwa mazungumzo tangu asubuhi kwenye ikulu ya rais, wamekubaliana na jina la Moustapha Adib, 48, balozi wa Lebanon nchini Ujerumani tangu mwaka 2013.

Jina l balozi huyo ambaye hafahamiki sana katika ulingo wa kisiasa nchini Lebanon lilipendekezwa Jumapili jioni na vigogo wa kisiasa wa madhehebu ya Sunni, akiwemo waziri mkuu wa zamani Saad Hariri.

Hata hivyo vuguvugu la maandamano nchini Lebanon liliipinga mara moja likisema uteuzi wa Moustapha Adib unakwenda kinyume na mabadiliko wanayoyataka.

Viongozi kutoka Magharibi wameitikia wito wa Walebanon wa kutaka mabadiliko makubwa ya kisiasa baada ya mlipuko katika bandari ya Beirut ambao ulisababisha takriban watu 188 kupoteza maisha, na ambapo wanasiasa walitwikwa lawama kwa uzembe na ufisadi.