LEBANON-SIASA-USALAMA

Rais Aoun ataka kutangazwa kwa 'taifa lisiloegemea dini' nchini Lebanon

Rais wa Lebanon Michel Aoun wakati wa hotuba yake katika ikulu ya ya huko Baabda, Agosti 30, 2020.
Rais wa Lebanon Michel Aoun wakati wa hotuba yake katika ikulu ya ya huko Baabda, Agosti 30, 2020. Dalati Nohra/Handout via REUTERS

Rais wa Lebanon Michel Aoun amekiri haja la kubadili mfumo wa kisiasa nchini Lebanon na kutaka kutangazwa kwa 'taifa lisiloegemea dini' nchini humo katika mkesha wa ziara ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ambaye amekuwa akitoa shinikizo juu ya mabadiliko ya mfumo wa dini.

Matangazo ya kibiashara

"Kwa sababu nina uhakika kwamba taifa lisiloegemea dini lina uwezo wa kulinda raia wote, na kudumisha umoja wa wananchi, naomba Lebanon itangazwe kama taifa lisiloegemea dini", amesema rais wa Lebanon katika hotuba yake.

Rais Michel Aoun hadi sasa alikuwa hataki kusikia madai ya maandamano yaliyozuka Oktoba 2019. Jumapili jioni, aliahidi "kutoa wito wa mazungumzo kati ya viongozi wa kidini na viongozi wa kisiasa ili wafikie hatua inayokubalika na wote ”ambayo itawezesha marekebisho ya katiba.

Emmanuel Macron, kiongozi wa kwanza wa kigeni kuzuru Lebanon baada ya mlipuko uliosababisha vifo vingi katika bandari ya Beirut, alikuwa amewasihi wanasiasa wa nchi hiyo kufanya mageuzi muhimu ya kisiasa.

Viongozi kutoka Magharibi wameitikia wito wa Walebanon wa kutaka mabadiliko makubwa ya kisiasa baada ya mlipuko katika bandari ya Beirut ambao ulisababisha takriban watu 188 kupoteza maisha, na ambapo wanasiasa walitwikwa lawama kwa uzembe na ufisadi.