AFGHANISTANI-TALIBAN-USALAMA

Mazungumzo ya amani: Wajumbe wa serikali ya Afghanistan wasubiriwa Qatar siku ya Alhamisi

Mjumbe mkuu wa Taliban katika mazungumzo na serikali ya Kabul, Mullah Abdul Ghani Baradar, baada ya kutiwa saini kwa makubaliano ya Doha na Marekani Februari 29, 2020 katika mji mkuu wa Qatar.
Mjumbe mkuu wa Taliban katika mazungumzo na serikali ya Kabul, Mullah Abdul Ghani Baradar, baada ya kutiwa saini kwa makubaliano ya Doha na Marekani Februari 29, 2020 katika mji mkuu wa Qatar. GIUSEPPE CACACE / AFP

Wajumbe wa serikali ya Afghanistan katika mazungumzo ya amani nchini humo watasafiri kwenda Qatar siku ya Alhamisi, ambapo mazungumzo ya amani na waasi wa Taliban yatafanyika, msemaji wa Baraza Kuu la Maridhiano ya kitaifa amesema.Tarehe ya mazungumzo hayo haijatangazwa.

Matangazo ya kibiashara

Taliban wametaka kuachiliwa huru kwa kundi la mwisho la wafungwa 320 kabla ya mazungumzo yoyote. Kwa jumla ya idadi hii ya wafungwa wa Taliban,, serikali imewaachilia huru 200. Baadhi ya serikali za Magharibi zinapinga kuachuliwa huru kwa wafungwa 120 wanaobaki.

"Timu ya wajumbe wa serikali itaondoka kwenda Doha kesho Alhamisi," amesema Fraidoon Kwazoon, msemaji wa Abdallah Abdallah, ambaye anaongoza Baraza Kuu la Maridhiano ya kitaifa.

Wanamgambo 200 wa Taliban, waliokuwa wanazuiliwa katika gereza kuu huko Kabul, waliachiliwa huru Jumatatu na Jumanne wiki hii; wakati huo huo, kundi la Taliban limewaachilia huruaskari sita wa vikosi maalum vya Afghanistan.

"Tunataka kukamilisha zoezi hili la kubadilishana wafungwa ili mchakato wa amani uanze kutekelezwa haraka iwezekanavyo," amesema afisa mwandamizi wa serikali ya Afghanistan.

Zoezi hili la kubadilishana wafungwa ni sehemu kuu ya makubaliano yaliyomalizika mwezi Februari kati ya Marekani na Taliban juu ya kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani nchini afghanistan badala ya mazungumzo kati ya waasi na serikali ya Kabul.

Lakini hatua ya kuachiliwa kwa karibu wanamgambo 400 wa Taliban wenye msimamo mkali, waliohusika katika mashambulio ambayo yaligharimu maisha ya watu wengi nchini Afghanistan, ilizua mgongano katika serikali ya Kabul.