PALESTINA-MAZUNGUMZO-USALAMA-SIASA

Makundi hasimu Palestina yajadili mkataba wa Israeli na Umoja wa Falme za Kiarabu

Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas.
Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas. REUTERS

Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas amefanya mkutano wa nadra na makundi hasimu katika jaribio la kuweka umoja mbele baada ya makubaliano yaliyofikiwa mwezi uliopita kati ya Israeli na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ili kufufua uhusiano wao wa kidiplomasia.

Matangazo ya kibiashara

Mkutano huo ulifanyika kwa njia ya video kati ya Ramallah, katika Ukingo wa Magharibi, na mji mkuu wa Lebanon Beirut, ambapo mkuu wa Hamas Ismail Hanyeh na katibu mkuu wa Islamic Jihad Zyad al Nakhalah wanaishi.

Ni nadra kwa Fatah, chama cha Abbas, na Hamas kuwa na mawasiliano ya hali ya juu baada ya miaka kadhaa ya makabiliano.

Wapalestina walishangazwa na makubaliano ya "kurejesha uhusiano" yaliyofikiwa kati ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Israeli chini ya kivuli cha rais wa Marekani Donald Trump, wakiona mkataba huo ni usaliti ambao unaweza kudhoofisha msimamo wa muda mrefu wa nchi za Kiarabu zinazoitaka Israeli kuondoka kwenye maeneo inayoshikilia kimabavu.

Abbas amekataa kushirikiana na serikali ya Trump kwa zaidi ya miaka miwili, akiishutumu kwa upendeleo wa Israeli na kukataa mpango wa amani wa Mashariki ya Kati uliowasilishwa na Washington mwezi Januari mwaka huu.