Marekani yapunguza idadi ya wanajeshi wake nchini Iraq

Wanajeshi wa Marekani huko Kirkuk, kaskazini mwa Iraq, Machi 29, 2020.
Wanajeshi wa Marekani huko Kirkuk, kaskazini mwa Iraq, Machi 29, 2020. AHMAD AL-RUBAYE / AFP

Jeshi la Marekani limetangaza limefikia hatua ya kupunguza idadi ya wanajeshi wake waliopelekwa nchini Iraq, ambapo idadi ya wanajeshi itashuka kutoka kwa wanajeshi 5,200 hadi 3,000 ifikapo mwisho wa mwezi huu.

Matangazo ya kibiashara

Urasimishaji huu ulikuwa ukitarajiwa kwa muda mrefu. Shirika la habari la Reuters liliripoti mwezi uliopita kwamba Marekani itapunguza idadi ya wanajeshi wake nchini Iraq kwa karibu theluthi moja.

Vikosi vya Marekani vilivyopelekwa nchini Iraq vinachangia katika vita dhidi ya kundi la Islamic State (IS) lakini viongozi wa muungano wa kimataifa wanachukulia kuwa vikosi vya Iraq sasa vinaweza kudhibiti tishio hili peke yao.

"Tunaendelea kukuza mipango yetu ya ushirikiano ambayo inaimarisha vikosi vya Iraq na kutuwezesha kupunguza uwepo wetu nchini Iraq," amesema Jenerali wa kikosi cha majini Frank McKenzie, wakati wa ziara yake nchini Iraq.

Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye atawania katika uchaguzi wa urais wa Novemba 3, alifanya kampeni mwaka 2016 akiahidi kukomesha "vita visivyo na mwisho" vya Marekani, ambayo inaendelea kupunguza idadi ya wanajeshi wake katika nchi kama Afghanistan, Iraq na Syria.