KUWAIT-SIASA

Kuwait yampata mfalme mpya baada ya kifo cha Sheikh Sabah

Sheikh Nawaf al-Ahmad Al-Sabah, Mfalme mpya wa Kuwait akiapishwa mbele ya Bunge la taifa nchini Kuwait Septemba 30, 2020
Sheikh Nawaf al-Ahmad Al-Sabah, Mfalme mpya wa Kuwait akiapishwa mbele ya Bunge la taifa nchini Kuwait Septemba 30, 2020 AFP

Aliyekuwa mfalme wa Kuwait, Sheikh Sabah, alizikwa Jumatano nchini mwake siku moja baada ya kifo chake huko Marekani akiwa na umri wa miaka 91, na kaka Sheikh Nawaf al-Ahmad Al-Sabah ameapishwa kuchukuwa hatamu ya uongozi wa nchi hii tajiri ya mafuta ya Ghuba.

Matangazo ya kibiashara

"Naapa kwa jina la Allah, kuheshimu katiba na sheria za nchi, kulinda uhuru wote, maslahi na mali ya umma na kulinda uhuru na mamlaka ya mipaka ya nchi," alisema mfalme huyo mpya wakati akipishwa na bunge.

Sheikh Sabah, mpatanishi mzuri aliyechukuliwa kama mbunifu wa sera ya kigeni ya Kuwait, alitawala miaka 14. Alifariki dunia Jumanne huko Minnesota (kaskazini mwa Marekani) ambapo alikuwa amelazwa hospitalini tangu mwezi Julai.

Sheikh Sabah alizikwa katika makaburi ya Sulaibikhat katika mji mkuu.

Kulingana na kasri ya kifalme, watu walio karibu na mfalme huyo ndio waliruhusiwa kushiriki mazishi, hatua ambayo ilikusudia kuzuia umati mkubwa wakati huu janga la Corona likiendelea.

Nawaf aliteuliwa mrithi wa ufalme mwaka 2006, muda mfupi baada ya Sabah kuteuliwa kuongoza. Nawaf, ambaye alizaliwa Juni 25, 1937 katika mji mkuu wa Kuwait, alianza kazi ya siasa akiwa kwenye umri wa miaka 20, alipoteuliwa kuwa gavana wa mkoa wa Hawalli.