YEMEN-USALAMA-SIASA

Zaidi ya wafungwa wa kivita 1,000 waachiliwa Yemen

Wafungwa wa Yemeni wakiwasili katika uwanja wa ndege wa Sana'a kufuatia zoezi la kubadilishana wafungwa Alhamisi, Oktoba 15, 2020.
Wafungwa wa Yemeni wakiwasili katika uwanja wa ndege wa Sana'a kufuatia zoezi la kubadilishana wafungwa Alhamisi, Oktoba 15, 2020. AP Photo/Hani Mohammed

Zaidi ya wafungwa wa vita 1,000 wameachiliwa huru ndani ya muda wa saa 48 katika siku ya pili ya hatua ya kihistoria ya kubadilishana wafungwa kati ya pande mbili zinazozozana nchini Yemen chini ya mkataba uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa, shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (ICRC ).

Matangazo ya kibiashara

Zoezi hili la kubadilishana wafungwa wa kivita ni "kubwa zaidi tangu kuzuka kwa mzozo huo" mnamo mwaka 2014, imebaini ICRC, ambayo inashiriki operesheni hiyo. Siku ya Ijumaa, wafungwa 352 waliachiliwa na Alhamisi 704.

Zoezi hilo linaonekana kama hatua katika mchakato wa kisiasa kuelekea suluhu nchini Yemen, ambapo serikali, ikiungwa mkono na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, na waasi wa Houthi, wanaoungwa mkono na Iran, wanapigana.

Siku ya Ijumaa, ndege zilizokodiwa na ICRC zilisafirisha wafungwa kutoka Sanaa, mji mkuu wa Yemen unaoshikiliwa na waasi, kwenda Aden (kusini), ambako serikali inaendesha shughuli zake.

Siku moja kabla, ndege zilizobeba wafungwa wa kivita zilitua Sana'a, huko Seyoun, jiji la kusini mashariki linalodhibitiwa na serikali, na katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, ICRC imesema.

Wakati wa mazungumzo ya amani nchini Sweden mwaka 2018, serikali na waasi walikubaliana kubadilishana wafungwa 15,000 kwa jumla. Tangu wakati huo, mabadilishano ya wafungwa kati ya pande hizo mbili yamefanyika mara kwa mara.