Afghanistan: Ishirini na tano wauawa katika shambulio dhidi ya Chuo Kikuu cha Kabul
Watu wasiopungua ishirini na tano, ikiwa ni pamoja na wanafunzi, wameuawa leo Jumatatu na watu wenye silaha katika shambulio dhidi ya chuo kikuu cha Kabul, ikiwa ni shambulio la pili dhidi ya kituo cha elimu ndani ya siku kumi, viongozi na mashahidi wamesema.
Imechapishwa:
"Waliwapiga risasi wanafunzi wote waliowaona," Fathullah Moradi, aliyenusurika katika shambulio hilo na ambaye alifanikiwa kuwatoroka washambuliaji kwa kukimbia na kundi la marafiki kupitia moja ya vituo vya chuo kikuu, ameliambia shirika la habari la REUTERS.
Picha zilizorushwa hewani na afisa mwandamizi wa serikali zinaonyesha wanafunzi wakiwa wamelala sakafuni madarasani, wengine wakiwa bado wameshikilia vitabu. Mwanafunzi mwingine anaonekana akipigwa risasi wakati akijaribu kutoroka kupitia dirishani.
Baada ya mapigano yaliyodumu saa kadhaa kwenye chuo kikuu hicho, vikosi vya usalama vilifaulu kuwapiga risasi watatu kati ya washambuliaji hao, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani Tarik Arian amesema.
Awali Tarik Arian alisema kuwa watu 19 waliuawa na wengine 22 walijeruhiwa.
Kundi la Taliban, ambalo lilianzisha mazungumzo ya amani na serikali nchini Qatar bila hata hivyo kuweka chini silaha, limekana kuhusika na shambulio hilo na hakuna kundi lolote limedai kuhusika na shambulio hilo baya kabisa. Kulingana na mashuhuda, risasi zilitanguliwa na mlipuko.
Mwakilishi wa Jumuiya ya Kujihami ya nchi za Magharibi, NATO, nchini Afghanistan, Stefano Pontecorvo, amelaani shambulio hilo.
"Hili ni shambulio la pili kwa vituo vya elimu huko Kabul ndani ya muda wa siku 10. Watoto na vijana wa Afghanistan wanahitaji kujisikia wako salama kwenda shule," amesema katika taarifa.
Mwezi uliopita, watu wasiopungua 24 waliuawa katika shambulio la bomu la kujitoa mhanga katika kituo cha elimu huko Kabul, ambalo lilidaiwa kutekelezwa na kundi la Islamic State.