LEBANON

Lebanon: Mkutano wa misaada ya kibinadamu kujaribu kuokoa uchumi

Rais wa Lebanon, Michel Aoun, akiongoza moja ya vikao vya Serikali, nchi yake itakuwa mwenyeji wa mkutano wa ukusanyaji pesa za misaada
Rais wa Lebanon, Michel Aoun, akiongoza moja ya vikao vya Serikali, nchi yake itakuwa mwenyeji wa mkutano wa ukusanyaji pesa za misaada REUTERS/Mohamed Azakir

Ufaransa inaongoza mkutano wa misaada ya kibinadamu kwa Lebanoni ambao unatarajiwa kufanyika Jumatano hii, Desemba 2 alaasiri.

Matangazo ya kibiashara

Mkutano utafayika kwa njia ya video kwa sababu ya janga hatari la Covid-19.

Huu ni mpango wa Ufaransa kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa. Mkutano huu unalenga kuhamasisha washirika wa Lebanoni kuchangia fedha kwa nchi hiyo ambayo inapitia wakati mgumu na kukumbwa na mgogoro wa kiuchumi.

Mwezi Agosti mwaka huu, mara tu baada ya mlipuko mkubwa katika bandari ya mji wa Beirut, mkutano wa kwanza wa aina hii uliwezesha kupatikana euro milioni 250 za msaada wa dharura.

Jumatano wiki hii huko Paris, nchi za wafadhili, mashirika ya kimataifa na mashirika mengine yasiyokuwa ya kiserikali watakutana tena, wakati Lebanon inaendelea kutumbukia katika mgogoro.

Mfumuko wa bei, kushuka kwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo, madeni, ukosefu wa ajira, raia kukabiliwa na umasikini mkubwa ... Katika ripoti yake ya hivi karibuni Benki ya Dunia inaorodhesha takwimu za hali mbaya ya kiuchumi inayoikabili Lebanon kwa sababu ya 'kutokuwepo kwa makusudi kwa 'hatua madhubuti za kisiasa kwa upande wa mamlaka'.

Mamlaka inanyooshewa kidole nchini Lebanon, wakati kwa miezi kadhaa nchi hiyo inaendelea kutafuta serikali kwa hatari ya kuona viongozi wale wale wakisalia madarakani wakitoa matokeo kama hayo.

Walakini, hakutakuwa na mpango wa uokoaji wa uchumi kwa Lebanon bila mageuzi ya kina, wameonya wafadhili wa kimataifa wa nchi hiyo. Na nchi hii kwa leo inahitaji zaidi misaada ya dharura ya kibinadamu.